Mifugo yahatarisha Hifadhi ya Ruaha

21Sep 2020
Beatrice Shayo
MBEYA
Nipashe
Mifugo yahatarisha Hifadhi ya Ruaha

HIFADHI ya Taifa ya Ruaha Kanda ya Kusini inakabiliwa na changamoto ya wafugaji kuingiza mifugo katika hifadhi hiyo, hali ambayo inahatarisha usalama wa wanyamapori.

ng'ombe.

Hayo yalisemwa na Kamshina Msaidizi wa Hifadhi Kanda ya Kusini, Pius Mzimbe, akihojiwa na waandishi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) katika ziara iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).

Mzimbe alisema moja ya changamoto kubwa ambayo inawakabili ni wafugaji hao kuingiza mifugo ndani ya hifadhi wakiamini kuwa chakula kilichopo kwenye hifadhi hiyo kinanenepesha mifugo yao.

Alisema athari ya kuingiza mifugo ndani ya hifadhi ni kupata maradhi kwa wanyamapori wa hifadhi ama kusambaza magonjwa kwa wanyama waliopo nje ya hifadhi kikiwamo kimeta.

Alisema mbali na changamoto hiyo kumekuwa na tatizo jingine la uvunaji haramu wa samaki katika hifadhi kinyume cha sheria za hifadhi.

Alisema njia mbadala ya kuzuia uvuvi haramu wa samaki ni wananchi kutengenezewa mabwawa ili waache kuvuna samaki.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, alisema wanachokifanya ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na uhifadhi ili wananchi waelewe umuhimi wa hifadhi.

Alisema wananchi hao wanatakiwa kujua mwingiliano wa wanyama kwenda kwenye hifadhi kunaweza kusababisha magonjwa.

"Mwingiliano ukitokea basi ni madhara kwa hifadhi na kwa mifugo ambayo inaingizwa katika hifadhi, kikubwa tunachokifanya ni elimu unajua mnyama hana mipaka ingawa hifadhi zina mipaka," alisema.

Alisema ni muhimu wananchi wakaacha kuingiza mifugo katika hifadhi la sivyo watawachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Aidha, aliwataka wananchi kuonyesha maeneo ambayo watawekewa mabwawa ya samaki badala ya kuendelea kufanya ujangili wa samaki kwenye hifadhi.

Habari Kubwa