Mifuko ya uwezeshaji kuelimisha wananchi kwa maonyesho

10Apr 2017
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Mifuko ya uwezeshaji kuelimisha wananchi kwa maonyesho

WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa, anatarajia kufungua maonyesho ya mifuko ya uwezeshaji kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi.

WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa.

Maonyesho hayo yanayotarajiwa kufanyika mkoani Dodoma Aprili 18 hadi 22 mwaka huu yatawawezesha wananchi kujua kuhusu huduma zitolewazo na mifuko ya uwezeshaji nchini.

Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’I Issa, alisema maonyesho hayo ni ya kwanza kufanyika nchini na kwamba wananchi watapata fursa ya kuifahamu mifuko ya 19 ya serikali ambayo hutoa mitaji yenye masharti nafuu kwa Watanzania.

Aliitaja mifuko itakayoshiriki kuwa ni Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali, Mfuko wa Uwezeshaji Mwananchi, Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mfuko wa Dhamana za Mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

Mingine ni Mfuko wa Dhamana za Mikopo kwa Mauzo ya Nje ya Nchi,  Mfuko ya Kuwasaidia Makandarasi, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Mfuko wa Misitu Tanzania, SELF Microfinance Fund na Mfuko wa Kusaidia Kilimo na PASS Trust Fund.

“Lengo la kufanya maonyesho hayo ni kukidhi kiu ya Watanzania ya kupata mitaji yenye masharti nafuu, pia kuwaona wajasiriamali wa sekta mbalimbali walionufaika na mifuko hii uwezeshaji,”  alisema Issa.

Alisema kwamba kauli mbiu ya maonyesho hayo mwaka huu ni ‘Wezesha wananchi kiuchumi ili kujenga uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda’.  

Mhasibu Mkuu wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF), Ahazi Kibona, alisema mfuko huo unatoa mikopo kwa vijana wahitimu wa vyuo vya ufundi na vile vilivyosajiliwa na VETA, ili  kuwawezesha kukuza ujuzi wao.

Alisema kwa kipindi cha miaka miwili tangu mfuko huo uanzishwa, umeshatoa mkopo wa Sh. bilioni 1.4 kwenye mikoa mbalimbali na pia mafunzo kwa vijana 1,592 yatatolewa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Pembejeo na Zana za Kilimo wa Taifa (AGITF), Mariam Nkumbi, alisema mfuko unatoa mikopo ya pembejeo, kilimo, zana za kilimo na vifaa vya umwagiliaji kwa wakulima wadogo, taasisi, watu binafsi na walioko kwenye vikundi.

“Mfuko huu hufanya kazi nchi nzima na hadi sasa tumetoa mikopo ya matrekta 100 tangu uanze,” alieleza Nkumbi.

Habari Kubwa