Miili ya marehemu wa ajali ya basi New Force yatambuliwa

22Sep 2016
Furaha Eliab
Njombe
Nipashe
Miili ya marehemu wa ajali ya basi New Force yatambuliwa

MIILI yote 12 ya watu waliofariki dunia katika ajali ya basi la New Force iliyotokea Septemba 19, mwaka huu mkoani Njombe imechukuliwa na ndugu zao kwa maziko.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kibena, Dk. Francis Benedict, alisema kati ya miili hiyo, tisa imesafirishwa kuelekea mkoani Ruvuma, miwili kuelekea jijini Dar es Salaam na mmoja mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Dk. Benedict aliwataja marehemu waliotambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa maziko kuwa ni Beteina Mhenga, mkazi wa Songea, Prottesa Mwingira, mkazi wa Peramiho na Maria Mapunga (4), wakazi wa Peramiho, Salma Njovu (50) na Pets Ngonyani (8), wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Wengine ni Angela Juate Morres (25), mkazi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, Reuben Matembo (45), mkazi wa jijini Dar es Salaam, Hellena Chale (25), mkazi wa Songea, Hossana Mbuesa (20), mkazi wa Songea, Nurdini Mpunga, mkazi wa Songea na mmoja ambaye bado jina lake halijafahamika.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi,
alifika Hospitali ya Kibena, kuwapa pole ndugu waliokuwa wakiitambua miili ya wapendwa wao na kuichukua kwa maziko.
Aidha, Dk. Benedict alisema kuwa hali ya majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa hospitali hapo zinaendelea vizuri huku wengine wakiruhusiwa kurejea nyumbani kwao.

Hata hivyo, alisema majeruhi sita kati yao wanawake wanne na wanaume wawili, bado wanaendelea na matibabu.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, amewaonya madereva kuwa waangalifu na kuacha kwenda mwendokasi hasa katika maeneo ambayo askari wa usalama barabarani hawapo.

"Imekuwa ni tabia kwa madereva wengi kuendesha magari kwa mwendokasi wanapofika maeneo ambayo hakuna polisi. Tuna taarifa kuwa kila wanapoondoka Songea, madereva huendesha magari yao kwa mwendo kasi kabla ya kufika mjini Njombe, na wanapokwenda Songea wakifika Kifanya, huongeza mwendo," alisema Dk. Nchimbi.

Habari Kubwa