Mijadala itakayozua mvutano Ukawa, CCM bungeni yafika

07Nov 2016
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Mijadala itakayozua mvutano Ukawa, CCM bungeni yafika

MKUTANO wa tano wa Bunge la 11 leo unaingia wiki la pili, huku miradi inayohisiwa kuwa na ufujaji wa mabilioni ya shilingi katika sekta mbalimbali ikitarajiwa kujadiliwa.

Miradi hiyo itajadiliwa wakati Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali Mitaa (LAAC) zitakapowasilisha ripoti zake bungeni kesho na keshokutwa.

Ratiba ya vikao vya Bunge inaonyesha kesho na keshokutwa, kamati hizo nyeti zitawasilisha bungeni ripoti zake za uchambuzi kuhusu ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2014/15.

Mijadala inayohusu ripoti za CAG, mara nyingi huzua mvutano baina ya wabunge wa chama tawala cha CCM na wale wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanaounda pia kambi kuu ya upinzani.

Aprili 24, CAG, Prof. Mussa Juma Assad, alifika kwenye ofisi za Bunge na kukabidhi ripoti zake za ukaguzi kwa kamati hizo nyeti zikionyesha ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi katika baadhi ya taasisi na mashirika ya umma.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni siku hiyo, Prof. Assad alisema ofisi yake katika mwaka wa fedha 2014/15, ilifanya ukaguzi kwenye taasisi 199 za Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa 164 na Mashirika ya Umma 102 kati ya mashirika 186.

Aidha, alisema ofisi yake ilifanya ukaguzi kwenye miradi ya maendeleo 799, hivyo kufanya idadi ya ripoti za ukaguzi wa fedha zilizotolewa, kufikia 1,264.

Mbali na utekelezaji duni wa bajeti ya Sh. trilioni 6.45 iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, ripoti za CAG zinaonyesha kukua kwa kasi kwa Deni la Taifa hadi kufikia trilioni 33.5 Juni 30, 2015, likiwa ni ongezeko la asilimia 27 kutoka Sh. trilioni 26.49 Juni 30, 2014.

Ripoti za CAG pia zinaonyesha udhaifu katika usimamizi wa rasilimali watu kutokana na uwapo wa watumishi hewa na changamoto katika ununuzi na usimamizi wa mikataba pamoja na matumizi yanayofanyika nje ya bajeti.

Udhaifu katika usimamizi wa mali na madeni na changamoto katika urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wanufaika umebainishwa pia katika ripoti za CAG.

Baadhi ya taasisi na mashirika ambayo yalibainika kuwa na matatizo ya utumiaji fedha za umma katika ripoti hizo za CAG ni pamoja na Shirika la Ndege (ATCL) ambalo linaendeshwa kwa hasara na Mamlaka ya Bandari (TPA) iliyobainika kuwa na mita za kupima mafuta zisizotumika, uchakavu wa karakana ya meli, kukosekana kwa mfumo wa kutambua makontena na kutoonekana kwa meli 85 zilizotia nanga katika mfumo wa mapato ya mamlaka hiyo.

Taasisi nyingine ni Mamlaka ya Mapato (TRA) ambayo ilionekana mfumo wake uko tofauti na ule wa TPA katika ukusanyaji mapato, Kampuni ya Simu (TCCL) iliyobainika kujiendesha kwa hasara kwa muda mrefu (jumla ya Sh. bilioni 361 kufikia mwaka 2014), Mamlaka ya Chakula na Dawa ambayo iligundulika kuingiza dawa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 2.3 (Sh. bilioni 4.6) bila kuzifanyia ukaguzi na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambayo ukaguzi ulibaini kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi kutokana na kutolipia dawa bandarini.

Ripoti za CAG pia zinaonyesha udhaifu katika baadhi ya mikataba ya Mamlaka ya Udhibiti wa Anga (TCAA) huku Benki ya Maendeleo (TIB) ikibainika ina changamoto za wakopaji kutorejesha fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali.

Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirika la Utangazaji (TBC) pia yamebainishwa katika ripoti za CAG kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

Mashirika mengine 'yaliyoanikwa' kwenye ripoti za CAG ni Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF) na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) huku miradi ya maji, elimu, gesi asilia na tathmini ya athari za mazingira nayo ikitajwa kukumbwa na changamoto za ubadhirifu wa fedha.

Ripoti hizo pia zinaonyesha matumizi mabaya ya fedha katika halmashauri mbalimbali, fedha za mfuko wa vijana na wanawake zikionekana kuziumbua halmashauri nyingi.

VYAMA VYA SIASA 'JIPU'
Ripoti za CAG pia zinaonyesha kati ya vyama 22 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, ni kimoja tu kilichokuwa kimewasilisha hesabu zake kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2015, jambo ambalo ni kinyume cha Kifungu Na. 14 cha Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya Mwaka 1992.

SAKATA LA LUGUMI
Mbali na uchambuzi wa ripoti hizo, PAC pia inatarajiwa kutoa ripoti yake ya uchunguzi kuhusu sakata la utekelezaji wa mkataba tata kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd.

Kampuni hiyo ilikuwa inatekeleza mkataba wenye thamani ya Sh. bilioni 37 wa kufunga mashine za utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi 108 nchini, fedha zilizoidhinishwa katika bajeti ya mwaka 2011/12.

MISHAHARA KUBORESHWA?
Ratiba ya Bunge pia inaonyesha katika kikao cha leo, kutakuwa na Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2016.

Katika muswada huo, baadhi ya marekebisho yanayotarajiwa kufanyika ni mapendekezo ya marekebisho katika Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298.

Sehemu ya muswada huo inaeleza kuwa marekebisho hayo yamelenga kutoa tafsiri ya 'Recruitment Secretariat', maneno haya yametumika katika Sheria lakini hayakuwa yamepewa tafsiri.

"Kifungu cha 8 kinapendekeza kufanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka Katibu Mkuu (Utumishi) kurekebisha na kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi wa umma," sehemu ya muswada huo inasomeka.

"Sehemu hii pia inapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 9A kinachozizuia taasisi za umma, wakala, bodi na tume zisirekebishe au kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi.

"Kifungu kipya cha 9B kinachopendekezwa kinakusudia kuipa nguvu Sheria ya Utumishi wa Umma pale itakapokinzana na sheria nyingine kwenye mambo yanayohusu mishahara, posho na marupurupu ya watumishi."

Habari Kubwa