Mikakati yawekwa kudhibiti mlipuko wa ebola Kigoma

07Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
KIGOMA
Nipashe
Mikakati yawekwa kudhibiti mlipuko wa ebola Kigoma

MKOA wa Kigoma umetajwa kuwa ni moja ya mikoa iliyoko hatarini wakazi wake kupata mambukizi ya virusi vya ugonjwa wa ebola.

Mtoa huduma wa ugojwa wa Ebola akipuliziwa dawa kwenye ngoa yake(aliye vaa vazi la rangi ya njano)

Hali hiyo inatokana na kupakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) inayokabiliwa na ongezeko la watu 2,673 walioathiriwa na ugonjwa huo kuanzia  Agasti, 2018, huku  watu 1,823 wakipoteza maisha  tangu Julai 31, mwaka huu, sawa na asilimia 67% ya watu walioathiriwa na ugonjwa huo.

Kutokana na mwingiliano wa shughuli za kibiashara na undugu kwa baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kigoma, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, serikali imeratibu zoezi la aina ya mazoezi, mafunzo, ufuatiliaji na tathmini ya uwezo wa utoaji majawabu endapo ugonjwa utaingia mkoani hapa.

Lengo ni kukabiliana na uwezekano wa mlipuko wa  ugonjwa huo. 

Mkurugenzi Msaidizi Utafiti na Mipango Utawala na Maafa katika  Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashiru Taratibu, alieleza kuwa ofisi hiyo inasimamia kitengo cha maafa, ambapo zoezi la utayari linafanywa kwa mfumo wa afya awamu ya kwanza ambao unatekelezwa katika mikoa ambayo kuna uwezekano wa  kupata mambukizi ikiwamo Kagera, Kigoma na Mwanza.

"Wadau mbalimbali wa afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Mifugo na wadau mtambuka tudhibiti kabla ya kuingia kwetu,” alisema na kuongeza kuwa  lengo la serikali ni kudhibiti maeneo ya mipakani.

 “Sasa wataalamu wamepewa mafunzo, tunataka tuone matokeo ya mafunzo, ili kubaini mapungufu ya waliopata mafunzo kwa kuyaboresha, Kigoma, Mwanza na Kagera, ambayo  ni mikoa iliyoko hatarini kupata maambukizi ya virusi vya ebola,” alisisitiza Taratibu.

Mtaalamu wa Masuala ya Afya ya Jamii na Dharura Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faraja Mwaseja, alisema zoezi hilo litaanza kilitarajiwa kuanza juzi hadi Ijumaa.

Ofisa Afya mwandamizi wa Wizara ya Afya, Remidius Kakulu, alisema changamoto kubwa Kigoma ni kutokana na mwingiliano wa watu kutoka DRC na Burundi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Paul Chaote, alikiri kuwa mkoa huo una changamoto ya baadhi ya mipaka kuwa wazi hususan njia zisizo rasmi kuna uwezekano wa ugonjwa huo kulipuka.

 

 

 

 

Habari Kubwa