Mikopo elimu juu kaa la moto

11Dec 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mikopo elimu juu kaa la moto

MTANDAO wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) umesema kama serikali haitaingilia kati kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, mamia watashindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa haki hiyo.

Katibu wa TSNP, Joseph Malekela, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia kuhusu changamoto ambazo wanafunzi wanazipitia kwa sasa, huku baadhi wakikosa mikopo na wengine kulipwa kwa kupunjwa.

Akizungumzia rufani za wanafunzi walizokata Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) zilizotoka Jumamosi, Malekela alisema zaidi ya wanafunzi 600 ndiyo wameshinda.

“Katika taarifa ya bodi imeonyesha zaidi ya wanafunzi 600 wameshinda rufani zao za mikopo baada ya kukosa awali, kwa bahati mbaya Bodi ya Mikopo haijasema ni wanafunzi wangapi walikata rufani hizo,” alisema.

Malekela alisema wasiwasi walionao kama mtandao ni kwamba wanafunzi wengi waliokata rufani na hawajashinda, watashindwa kuendelea na masomo yao licha ya kuwa na uhitaji wa kupata fedha hizo.

“Tunataka kuwe na uwazi… ni wangapi walikata rufani na kwa nini wachache wamepata, na hao wengine ambao idadi yao hatujaelezwa wamekosa,” alisema.

Malekela alisema mtandao unataka kufanyike mapitio ya rufani hizo kwa sababu wapo wanafunzi ambao ni yatima, na wengine wenye mzazi mmoja na wenye ulemavu ambao kwa sasa hawajui hatima yao baada ya mchakato huo kutolewa.

Pia alisema jambo lingine ni kuhusu wanafunzi ambao wanaendelea na masomo na wana sifa ya kupata, lakini baadhi bado fedha zao hawajapata.

“Wanafunzi hawa wapo chuoni na sasa ni zaidi ya mwezi, lakini fedha za chakula, malazi wala ada hazijaletwa, tumefuatilia wanasema mwanafunzi aliyehama mafunzo yake wanasubiri TCU (Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania) iwathibitishe.

“TCU na Bodi ya Mikopo zote ni taasisi za serikali, suala la kupata uthibitisho kwamba mwanafunzi huyu alihama mafunzo ni suala la sekunde, tunasikitishwa na huu urasimu ambao mwisho wa siku unaosababisha maisha ya wanafunzi kuwa magumu.”

Malekela aliitaka serikali iingilie suala hilo kwa sababu wanafunzi wengi hawajui nini hatima yao ya masomo.

“Suala lingine linahusu, fedha za wanafunzi wanaostahili kupata mikopo, lakini zimekatwa, mapema mwezi huu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alizungumza kwamba kumekuwa na changamoto ndani ya bodi ya mikopo,” alisema.

Alisema naibu huyo alieleza kuwa changamoto hiyo kimtandao ilisababisha kukatokea kutawanywa baadhi ya fedha za wanafunzi na wengine kupata kidogo.

“Tangu naibu waziri azungumze sasa ni mwezi na wanafunzi hawajui nini hatima yao, tunataka suala hili lifanyiwe kazi kwa haraka kwa sababu hizi ni stahiki za wanafunzi na hazijawekwa kama mapambo ni matumizi ya watu ambayo mwisho wa siku zinawasaidia kielimu,” alisema.

Alisema ipo haja ya kufanyika mapitio upya kwa sababu wanafunzi wengi wamekuwa wakiacha masomo kwa kukosa ada.

“Wanafunzi wakishindwa kulipa ada wanashindwa kufanya mitihani na kushindwa kuendelea na vyuo vikuu, serikali ione umuhimu wa kusaidia hili.

“Namna bora ya kukabiliana na changamoto hizi ni kugharamia mahitaji ya wanafunzi ambayo ni ada, fedha hizi ambazo zimetolewa kwa wachache, wakienda kwa mtindo wa kulipa ada kila mwanafunzi hataachwa nyuma.”

“Mtandao unataka serikali iliangalia suala hili ili mwisho wa siku wanafunzi wote wanaostahili kupata mikopo wapate,” alisema.

Habari Kubwa