Mil. 57/- zatumika kuokoa watoto njiti

03Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Bunda
Nipashe
Mil. 57/- zatumika kuokoa watoto njiti

TAASISI ya Vodacom Tanzania, imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. milioni 57.8 kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) katika Hospitali ya St. Mary's iliyopo Kibara wilayani Bunda.

Akikabidhi vifaa hivyo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Rosalynn Mworia, alisema jukumu la taasisi hiyo ni kurudisha tabasamu kwa jamii, hivyo kutoa vifaa tiba kwa ajili ya watoto njiti ni faraja kwa taasisi yake.

"Tunafuraha kuwa sehemu ya kuokoa maisha kwa watoto njiti, maana vifaa tiba hivi vitawasaidia kuendelea kuishi na hivyo kutimiza ndoto na malengo yao hapo baadaye," alisema Mworia.

Alisema kati ya malengo ya Taasisi ya Vodacom Tanzania ni kuokoa maisha ya kinamama na watoto, ndio maana wamekuwa mstari wa mbele katika kuunga juhudi za serikali katika kutokomeza vifo vya mama na watoto nchini.

Mchango wa vifaa tiba ulijumuisha vifaa vya kuokoa maisha kama oksijeni ambavyo vitasaidia watoto njiti kupumua, viongeza joto kwa ajili ya kuhifadhi watoto hao, mashine za tiba mwanga (phototherapy machine) na mashine maalum za kupimia mapigo ya moyo, vitanda vinne, shuka 50 na mablanketi 20.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Renatusa Nkwande, aliishukuru taasisi hiyo kwa kazi wanayofanya na kwamba wana imani kuwa vifaa vilivyokabidhiwa hospitalini hapo vitatumika kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa watu wengi hususani kinamama na watoto wilayani humo.

Habari Kubwa