Milioni 7 kunufaika mpango wa TASAF

11Jul 2020
Welingtone Masele
Tabora
Nipashe
Milioni 7 kunufaika mpango wa TASAF

ZAIDI ya watu milioni saba wanaotoka katika kaya maskini nchini, wanatarajiwa kunufaika na mpango wa serikali wa kuwezesha kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Hayo yalibainishwa jana na Ofisa wa Mfuko huo kutoka Makao Makuu, Grace-Anna Maganga, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku nne ya kuhakiki taarifa za wanufaika wa mpango huo kwa wasimamizi wilayani Sikonge kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga.

Alisema kipindi cha pili cha awamu ya tatu (TASAF III) ya mpango huo, kinatarajia kufikia kaya maskini milioni 1,450,000 zenye zaidi ya watu milioni saba katika vijiji na mitaa ya halmashauri zote nchini ili kuboresha hali zao kiuchumi.

Maganga alibainisha kuwa mkazo mkubwa katika awamu hii utakuwa kuwezesha kaya zote zitakazoandikishwa kufanya kazi ili kujiongezea kipato ikiwamo kuongeza na kuboresha huduma za kijamii katika halmashauri zote 187 zilizopo nchini.

Kwa wa Maganga, mafunzo hayo yamelenga kuwapa mbinu za uhakiki wa walengwa wa mfuko huo utakaofanyika nchini kote ili kuondoa kaya zote za walengwa ambazo zimepoteza sifa.

“Utekelezaji wa mfuko huo katika awamu ya kwanza umepunguza umaskini wa mahitaji ya msingi kwa kaya kwa asilimia 10 na umaskini uliokithiri pia umepungua kwa asilimia 12,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Peresi Magiri, alipongeza serikali kwa kuanzisha awamu ya pili ya mpango huo kwa kuwa utasaidia kuboresha maisha ya wananchi wanaotoka katika familia maskini wilayani hapa.

Aliongeza kuwa, katika awamu ya kwanza ya mpango huo, vijiji 46 kati ya 71 vilivyoko katika wilaya hiyo vilinufaika lakini
awamu hii ya tatu vijiji vyote nchini, ikiwemo vya Sikonge, vitanufaika.

Mratibu wa TASAF wilayani Sikonge, Claud Nkanwa, alisema uhakiki wa walengwa umekuja wakati mwafaka kwa kuwa kaya maskini nyingi zimekuwa zikilalamika kutoingizwa katika mpango wakati zilistahili.

Aliongeza kuwa awamu ya pili ya mpango huo ni mkombozi kwa wakazi wa wilaya hiyo kwa kuwa utasaidia kuinua kaya maskini
kiuchumi ikiwamo kutoa ajira za muda mfupi kwa makundi mbalimbali ya kijamii yenye hali duni kimaisha.

Habari Kubwa