Milvik Tanzania yapata tuzo ya huduma bora ya bima

09Oct 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Milvik Tanzania yapata tuzo ya huduma bora ya bima

KAMPUNI ya MILVIK Tanzania imepata tuzo ya Huduma ya Bima yenye Ubunifu Zaidi kupitia huduma yake ya Bima Mkononi, inayopatikana kwa watumiaji wa Tigo Pesa nchini.

Meneja Mkuu wa Milvik, Berengere Lavisse akipokea tuzo.

Tuzo hiyo ilitolea na Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima (Tira), katika hafla iliyofanyika jijini Mwanza ya tuzo za bima mwaka 2019.

 Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Meneja Mkuu wa Milvik, Berengere Lavisse,  alisema  wanajivunia kutoa huduma rahisi na nafuu kwa wateja wa kipato cha chini kwa ushirikiano na Tigo Pesa, Resolution na Mo.

“Kupitia bima yetu mpya ya Kulazwa na Watoto, wazazi wanaweza kuwalinda watoto wao kwa matibabu ya kulazwa kwa Sh. 750 tu kwa mwezi kwa kila mtoto, kwa kutumia simu zao, bila kujaza fomu za makaratasi na kwa mfumo rahisi wa malipo kupitia Tigo Pesa,” Lavisse alisema.

Aliongeza kuwa “Tunawashukuru wateja wetu ambao wameendelea kutuamini katika kulinda hatima za familia zao na tunatarajia kuwaletea huduma zenye ubunifu zaidi katika mwaka 2020.”

Akizungumzia bima hiyo, alisema wana Bima Mkononi ya Kulazwa Sh. 1,500 kwa mwezi, Bima Mkononi ya Ajali Binafsi Sh. 1,000 na Bima Mkononi ya Maisha Sh 1,500, au kifurushi chenye bima zote kiitwacho Bima Mkononi Faraja Yangu.

“Mnamo Mei mwaka huu, Milvik ilizindua mfumo mpya wa malipo unaowezesha wateja kukatwa malipo kila mwezi kutoka kwenye akaunti zao za Tigo Pesa na kuifanya Bima Mkononi kuwa huduma ya gharama nafuu na rahisi kutumia kwa watumiaji wa kipato cha chini,” Lavisse alisema.

Alisema wateja wanaweza kujinga kupitia simu yako ya mkononi kwa kupiga *148*15# au kupitia huduma kwa wateja kwa kupiga simu ya bure 0659071001.

Habari Kubwa