Mimba zakatisha masomo wanafunzi wengi Busega

11Apr 2017
Ahmed Makongo
BUSEGA
Nipashe
Mimba zakatisha masomo wanafunzi wengi Busega

TAKWIMU zinaonyesha kuwa, takribani wanafunzi 40 wa kike wanaojiunga na kidato cha kwanza katika wilaya ya Busega, mkoani Simiyu, kati yao 15 hadi 18 ukatisha masomo yao kwa sababu ya kupewa ujauzito kila mwaka.

Hayo yalisemwa na Mbunge wa Busega (CCM), Dk. Raphael Chegeni, wakati akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu juzi kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.

Akizungumzia hali ya elimu katika jimbo lake, Dk. Chegeni alisema wanafunzi wengi wa kike wamekuwa wakikatisha masomo yao kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali, wengi wao kutokana na kupatiwa ujauzito.

Alisema kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, yeye kama Mbunge ameanzisha mpango wa ujenzi wa hosteli za wasichana katika shule zilizoko pembezoni mwa jimbo hilo ili kuwanusuru watoto wa kike waweze kuendelea na masomo yao.

“Ni hali ya kutisha sana maana kati ya watoto 40 wanaoandikishwa kuanza kidato cha kwanza kati yao 15 hadi 18 hukatisha masomo yao kutokana na kupatiwa ujauzito. Nimeamua kuanzisha mkakati kabambe wa kujenga hosteli kwenye shule zilizoko pembezoni mwa jimbo letu ili tuweze kuwanusuru hawa watoto wetu wa kike,” alisema.

Alisema watoto wa kike wamekuwa wakienda ama kutoka shuleni kwa kutembea kwa miguu umbali mrefu na wakiwa njiani wamekuwa wakikumbana na vishawishi vingi kutoka kwa wanaume ambavyo huwaingiza kwenye mtego wa kufanya vitendo vya ngono na kupewa ujauzito na kukatisha masomo yao.

Dk. Chegeni alizitaja shule ambazo zimekwishaanza utekelezaji wa mradi huo wa hosteli za wasichana kuwa ni sekondari ya Ngasamo ambayo kwa miaka mingi watoto wa kike walikuwa wakikumbana na changamoto hiyo kwa sababu ya kutokuwapo kwa bweni la wasichana.

Alisema kuwa shule hiyo imekuwa ikipokea wanafunzi wa kata mbili za Imalamate na Ngasamo na kwamba mradi huo wa hosteli pia utatekelezwa katika shule nyingine jimboni humo.

Habari Kubwa