Mipaka mipya kiutawala kurejewa

12May 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mipaka mipya kiutawala kurejewa

BUNGE limeelezwa kuwa serikali inatambua umuhimu wa kufanya mapitio ya mipaka kwa baadhi ya mikoa, wilaya na majimbo ya uchaguzi hasa yenye mwingiliano unaosababisha ugumu wa utoaji wa huduma za jamii.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda, alisema jana bungeni mjini hapa  alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Vijijini (CCM), Martin Msuha.

Katika swali lake, Msuha alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya mipaka ya baadhi ya maeneo kama vile mikoa, wilaya na majimbo ya uchaguzi kwa kuwa baadhi ya mipaka ya maeneo hayo ina mwingiliano unaosababisha ugumu wa utoaji wa huduma za jamii.

“Je, serikali ina mpango gani wa kuligawa jimbo la Mbinga Vijijini kwa kuzingatia ukubwa wake wa kata 29?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Kakunda alisema kazi hiyo inaweza kusababisha mapendekezo ya maeneo mapya ya utawala na itafanyika baada ya kukamilisha miundombinu ya majengo ya ofisi, huduma mbalimbali na vifaa katika mikoa, wilaya na halmashauri mapya zilizoanzishwa tangu 2012.

Hata hivyo alisema kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa mamlaka ya kuyagawa majimbo ya uchaguzi.

Alisema mgawanyo huo unazingatia vigezo vya idadi ya watu, jiografia, hali ya mawasiliano , ukubwa wa jimbo na uwezo wa ukumbi wa Bunge.

“Ili jimbo lolote ligawanywe, Tume hutoa tangazo kuhusu nia hiyo, baada ya tangazo mapendekezo hujadiliwa katika vikao vya halmashauri, kamati ya ushauri ya wilaya na mkoa na hatimaye huwasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo hutangaza jimbo jipya baada ya kupata kibali cha Rais,”alisema.