Miradi ya bil. 114/- kuongeza maji Dar, Pwani

03Jul 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Miradi ya bil. 114/- kuongeza maji Dar, Pwani

MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), imetia saini mikataba sita na Benki ya Dunia pamoja na makandarasi yenye thamani ya Sh. bilioni 114 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam na Pwani.

Katika halfa hiyo iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam katika ofisi za DAWASA, ilihudhuliwa na kushuhudiwa na Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa; Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo; Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso; Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega; Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasa, Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange; Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Wakuu wa Wilaya na Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Waziri Mbarawa alisema katika miradi hiyo, Dawasa inatumia fedha zake za ndani Sh. bilioni 40 kati ya Sh. bilioni 114 kutekeleza miradi mitano kati ya sita, ambapo mmoja kati ya miradi hiyo umesainiwa na Benki ya Dunia.

Alisema mradi wa kwanza ni wa usambazaji wa maji kuanzia kwenye matangi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mpaka Bagamoyo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa mkopo nafuu ambao utekelezaji wake ni wa miezi 18 mpaka kukamilika.

Alisema kuwa mradi huo wa Chuo Kikuu hadi Bagamoyo unalenga kuhudumia wakazi zaidi 750,000 kulingana na usanifu ambapo wateja wapya zaidi 64,000 wa majumbani wataunganishwa na kuondoa tatizo la maji katika maeneo ya Changanyikeni, Bunju, Wazo, Ocean by Zone, Salasala, Bagamoyo zone na Vikawe zone katika wilaya za Bagamoyo, Ubungo na Kinondoni.

Mradi wa pili ni wa kusafirisha maji kutoka Jeti hadi Buza ambapo kazi ya ulazaji bomba la km.1.9 imekamilika na kipande kilichobaki cha km. 5.6 Dawasa itanunua bomba kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.

Mradi wa tatu ni wa uchimbaji wa visima 20 katika eneo la Kimbiji na Mpera ambavyo vitazalisha maji lita milioni 260 kwa siku, na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

Prof. Mbarawa alisema mradi wanne ni wa usambazaji wa maji kutoka Kisarawe-Pungu- Gongo la Mboto-Pugu Station-Airwing-Ukonga hadi Majohe ambao unatekelezwa na Mkandarasi Chico Limited kwa gharama ya Sh. bilioni 7, na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na maunganisho mapya zaidi ya 50,000 lengo la Dawasa ni kuhakikisha agizo la serikali linatekelezwa la kufikia asilimia 95 ifikapo Desemba mwaka huu ya upatikanaji wa maji.

Alisema mradi wa tano utatekelezwa katika mji wa Mkuranga ambapo hali ya upatikanaji wa maji sio wa kuridhisha kwani vyanzo vyote vya maji vimekauka, kusababisha wakazi wa mji huo kutumia maji yanayotiririka kutoka kisima kilichochimbwa na Dawasa mwaka 2015 kwa ajili ya utafiti.

“Hivi sasa mtandao wa mabomba ya maji uliopo wenye urefu wa Kilomita 11 unahudumia watu 4,500 kati ya watu zaidi ya 25,500,” alisema Prof. Mbarawa.

Aliongeza kuwa watu wa Dar es Salaam na Pwani wanahitaji maji, hivyo ni jukumu la Dawasa kuhakikisha wanasimamia vizuri utekelezaji wa mradi hiyo kwa kuwa itakuwa mkombozi kwa wananchi.

Alitaja mradi wa sita kuwa ni wa kusafirisha maji kutoka Mlandizi (Ruvu Juu) hadi kijiji cha Mboga (Chalinze), ambao utasaidia kuondoa kero ya maji katika maeneo hayo kutokana na kuongeza kwa watu na ujenzi wa viwanda unaoendelea katika eneo la Mboga.

“Mradi huu wa bomba kuu unatarajiwa kusafirisha kiasi cha lita za ujazo 9,300,000 kwa siku, ambazo zitakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi wapatao 120 kwa siku,” alisema Prof. Mbarawa.

Naye Jafo, alisema Waziri wa Maji anafanya kazi usiku na mchana kuhudumia wananchi na kuwataka viongozi wengine waache tabia ya kufanya maigizo katika kuhudumia wananchi kwani watu wana shida.

“Jana (juzi) tumeanzisha wakala wa maji vijijini na nataka nikuhakikishie tutatoa orodha ya makandarasi ambao sio waaminifu kwa kuwa kulikuwa na uhujumu mkubwa katika wizara yetu, watu walikuwa wanakuja kufanya kazi na sisi wakati hawana hata mtaji wa kutosha na mwisho wa siku wanaharibu kazi kwa kushindwa kutekeleza miradi kwa ufasaha,” alisema Aweso.

“Tunashuruku sana kukubali kuunganisha Mkuranga na Dawasa ili tuweze kuwahudumia na katika kuhakikisha wakazi wa Mkuranga wanapata majisafi na ya uhakika tumepeleka Sh. bilioni 5 kwa ajili ya mradi wa tangi kubwa ambapo pesa hizo ni kutoka katika mapato ya ndani,” alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja.