Mishahara, madeni yalamba tril. 12/- ndani ya miezi 10

15Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Mishahara, madeni yalamba tril. 12/- ndani ya miezi 10

SERIKALI imeliambia Bunge kuwa imefanikiwa kukusanya Sh. trilioni 12.9 kutokana na mapato ya kodi katika miezi 10 ya mwaka huu wa fedha kuanzia Julai, mwaka jana hadi Aprili, mwaka huu.

 

Hata hivyo, katika kipindi hicho cha miezi 10, serikali imetumia Sh. trilioni 12 kulipa mishahara ya watumishi wa umma na deni la serikali.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mipango, alipowasilishwa bungeni jijini Dodoma juzi mapendekezo kuhusu bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Dk. Mpango alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali ilitarajia kupata Sh. trilioni 32.48 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje.

Alibainisha kuwa hadi kufikia Aprili, mapato ya kodi yalifikia Sh. trilioni 12.9, sawa na asilimia 87.4 ya lengo wakati mapato yasiyo ya kodi yalifikia Sh. trilioni 2.04 (asilimia 122 ya lengo).

Alisema mapato yasiyo ya kodi yalivuka lengo kutokana na kuimarika kwa matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji maduhuli kwenye taasisi za serikali.

Alibainisha kuwa katika kipindi hicho, mapato ya halmashauri yalifikia Sh. bilioni 529.25, sawa na asilimia 72 ya lengo wakati misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ilifikia Sh. trilioni 1.7 (asilimia 86 ya lengo).

Waziri huyo alifafanua kuwa mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipia dhamana za serikali zilizoiva, ilifikia Sh. trilioni 33 (asilimia 57.4 ya lengo) na mikopo ya masharti kibiashara ya nje ilifikia Sh. bilioni 692.3.

"Kutofikiwa kwa malengo ya mapato ya kodi kulitokana na sababu mbalimbali, zikiwamo ugumu wa kutoza kodi sekta isiyo rasmi na kuendelea kuwapo kwa upotevu wa mapato kunakosababishwa tatizo la magendo hususan kupitia bandari bubu kwenye mwambao mrefu wa Bahari ya Hindi.

"Pia mwamko mdogo wa wananchi kudai risiti za kielektroniki wanapofanya ununuzi au baadhi ya wafanyabishara wasio waaminifu kutotoa risiti wanapofanya mauzo, Dk. Mpango,” alisema.

Aliongeza kuwa kutopatikana kwa mikopo ya ndani kama ilivyotarajiwa kumetokana na kupungua kwa washirika katika soko la fedha la ndani hususan mifuko ya hifadhi ya jamii iliyokuwa kwenye mchakato wa kuunganishwa.

Kwa upande wa mikopo ya nje ya kibiashara, Dk. Mpango alisema upungufu uliojitokeza ulitokana na hali ya masoko ya fedha ya kimataifa kubana zaidi hususan kuimarika kwa Dola ya Marekani na riba kubwa za mikopo.

"Hali hii pia ilisababisha majadiliano na taasisi za fedha za kimataifa kuchukua muda mrefu ili kuhakikisha serikali inapata mikopo hiyo kwa gharama zinazohimilika," alisema.

"Mwenendo wa upokeaji wa upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo baadhi ya washirika wa maendeleo kutotimiza ahadi zao kama walivyoahidi kwenye bajeti, kinyume cha misingi ya makubaliano yaliyoainishwa kwenye Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania (DCF), " alisema. 

TRIL. 12/- MISHAHARA, MADENI

Dk. Mpango alibainisha kuwa kati ya Sh. trilioni 22.19 zilizotolewa na serikali hadi kufikia Aprili mwaka huu, Sh. trilioni 6.3 zimetumika kulipa mishahara ya watumishi, ikiwa ni wastani wa Sh. bilioni 630 kwa mwezi.

Waziri huyo pia alisema serikali iliendelea kulipa madeni yake kwa mujibu wa mikataba, akibainisha katika kipindi hicho cha miezi 10, Sh. trilioni 5.7 zilitumika, ikiwa ni wastani wa Sh. bilioni 570 kwa mwezi. 

Kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Dk. Mpango alisema jumla ya Sh. trilioni 5.44 zilikuwa zimetolewa.

Aprili mwaka jana, waziri huyo aliwaambia waandishi wa habari bungeni jijini Dodoma kuwa serikali imekuwa ikishindwa kupeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo inayoidhinishwa na Bunge kutokana na kiwango kikubwa cha makusanyo yake kutumika kulipa mishahara ya watumishi wa Umma na Deni la Taifa.

Habari Kubwa