Misingi 5 ya mafanikio katika ajira na kazi

12May 2018
Kelvin Mwita
DAR ES SALAAM
Nipashe
Misingi 5 ya mafanikio katika ajira na kazi

MARA nyingi tukiwa hatuna ajira au kazi maalumu, hutamani kupata ajira hizo au kazi kwa lengo la kufikia malengo yetu ya kiuchumi na kijamii. 

Tunapopata ajira tunajikuta na hamasa kubwa inayotusukuma kutumia mbinu mbalimbali ili kufikia malengo yetu ya kiajira.  Cha kushangaza mara nyingi hamasa hii hupotea baada ya muda mfupi na kujikuta tunafanya kazi kwa lengo la kutimiza wajibu tu na kupata ujira.

 Wakati mwingine kazi hugeuka kama kero na kitu kinachochosha. Kuwa katika hali hii haimaanishi kuwa hatupendi kufanikiwa katika kazi na ajira zetu. 

Wengi huwa tunatamani kupata nafasi za uongozi, kupandishwa vyeo au kupata fursa mbalimbali zinazohusiana na kazi zetu. Lakini mara nyingi mafanikio haya na mengine yoyote katika ajira na kazi huwa hayaji hivi hivi bali yanahitaji mambo kadhaa ya kuzingatia ili kuyafikia. Mambo hayo ni;- 

BIDII

Bidii au juhudi katika shughuli yoyote ni moja ya vitu muhimu sana. Tunapoangalia mtendaji kazi mzuri katika ajira au kazi yake huwa tunatazama pia uwezo na juhudi anazoonyesha katika kufanikisha majukumu yake na kufikia malengo ya taasisi. 

Adui wa mafanikio katika ajira au kazi yoyote ni uvivu au kufanya kazi chini ya kiwango ya matakwa ya mwajiri wako. Jenga tabia ya kufanya kazi kwa bidii. Hakikisha kazi na majukumu yako yanafanywa kwa ubora na umakini mkubwa. 

Katika vitu ambavyo huangaliwa katika kutoa fursa kama vyeo, masomo na nafasi za uongozi ni bidii ya mtu binafsi anayoionyesha katika kuhakikisha taasisi inafikia malengo yake.

NIDHAMU

Bidii bila nidhamu inaweza ikafanya kila unachokifanya kikaonekana si lolote si chochote. Hebu jihoji unaishije ndani ya taasisi uliyopo? Watu wanakuona kama una nidhamu au mbambaishaji? 

Bila nidhamu hutaaminika hata kidogo na hiki ni kikwazo kikubwa sana katika maendeleo binafsi hasa yanayohusiana na kazi au ajira. Jenga tabia ya kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo. 

Hii ni moja ya sifa kubwa za viongozi na wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa. Nidhamu hupimwa hata kwa jinsi unavyoishi na wenzako ndani ya taasisi. Je, unawaheshimu na kuheshimu tofauti ziizopo kati yenu ikiwamo tofauti za kimawazo na kimtazamo?Usikubali kukwamishwa na vitu ambavyo ni vya kawaida kama hivi kwani vinatakiwa kufanywa na kila mtu mahali popote pale na si lazima kwenye kazi pekee. 

UJUZI NA MAARIFA

Ili kazi ifanywe vyema na kwa ufanisi, unahitaji uwezo wa kuifanya na uwezo huu hujengwa na ujuzi na maarifa. Kwa kuzingatia hili kuna haja ya kuhakikisha tunatafuta ujuzi na maarifa kila leo na kwa kila njia inayowezekana. Ukipata fura ya kwenda kusoma usiache kuitumia na ili kuipata kirahisi hakuna budi kuitafuta. 

Fanya juhudi za kuongeza maarifa yako ili kujiongezea thamani na uwezo. Kupata ujuzi na maarifa si lazima urudi shuleni pekee bali pia kwa kutafuta fursa zingine za kujiendeleza na kupata ujuzi na maarifa hayo katika mfumo usio rasmi. 

Hudhuria makongamano, semina na warsha mbalimbali, soma vitabu, vijarida na machapisho mbalimbali yanayotoa mbinu na maarifa yanayoweza kukuongezea uwezo wa kumudu vyema kazi yako. Tumia mitandao ya kijamii, tovuti na fursa mbalimbali katika intaneti ili kujifunza mambo yanayoweza kukupa maarifa zaidi na kukuongezea ujuzi.

MATUMIZI YA MUDA

Unautumiaje muda wako? Ni swali la kujiuliza kila siku. Muda ni kipimo kizuri sana cha kupima kwa namna gani tunapangilia mambo yetu na tunayafanikisha kwa wakati. 

Hakikisha unajua namna utakavyoutumia muda wako na kuliheshimu hilo. Jiwekee malengo muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kutumia muda kama kipimo chako na kuhakikisha unayafikia malengo hayo kwa wakati. 

Mfano unaweza kujiwekea hivi: “Leo ikifika saa nne asubuhi niwe nimeshamaliza kazi hii, ndani ya wiki hii nihakikishe nimeshamaliza ripoti na nmeikabidhi, miaka minne kuanzia sasa natakiwa niwe nmeshahitimu shahada ya uzamili” na kadhalika. 

Hii ni namna bora ya kujiwekea malengo kwa kutumia muda kama kipimo cha kujitathmini. Hakikisha unayaandika mahali, unayapitia mara kwa mara na unaonyesha jitiahada za kuyafikia. 

Heshimu na zingatia ratiba za taasisi na zako binafsi. Mambo madogo madogo kama kuwahi kazini yasiwe kikwazo katika mafanikio ya ajira na kazi yako. 

UPENDO

Watu watakutafsiri kwa kuzingatia ni kwa namna gani unahusiana na wengine. Wakiwa kwenye matatizo unachukua hatua gani? Je unawakimbia? Unawasema vibaya au unakuwa pamoja nao? Ukipata fursa kama ya uongozi unakuwa msaada kwa wengine au kikwazo kwao? 

Ni vyema kujitafakari na kujua nini tunafanya kwa ajili ya wengine. Mafanikio mahali popote yanakwenda pamoja na upendo kwa wengine. 

Ukishindwa kwenye hili ni dhahiri muda si mrefu utaanguka. Kuwa mfariji na msaada kwa wengine na uhakikishe unashiriki katika kuwainua wengine. Usitumie madaraka yako au fursa yoyote vibaya maana haya ni ya muda tu.

Jifunze kushirikiana na kila mtu bila ubaguzi kwenye shida na raha. Mwenzio anaumwa mtembelee na kama huwezi mpigie hata simu. Kama ana jambo la furaha jaribu kushiriki naye pia. 

Haya mambo madogo madogo yana uwezo wa kukuinua na kukufikisha mbali si katika mafanikio ya kazi na ajira pekee lakini hata katika mambo mengine ya kijamii. 

Wanaojishughulisha na watu hupendwa na watu, hivyo ni muhimu kujijengea ushawishi kupitia upendo. Kinyume cha upendo ni chuki, hiki ni cha kukiepuka kabisa kwa sababu hakijawahi kuwa na faida yoyote mahali popote.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, anapatikana kupitia 0659 08 18 38, [email protected], www.kelvinmwita.com