Misitu wakumbushwa kazi tu

27Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Misitu wakumbushwa kazi tu

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani amewataka watumishi wa Wakala wa Misitu (TFS) kuacha kufanya kazi kwa mazoea ya awamu za uongozi zilizopita.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.

Akifungua warsha kwa wadau wa mazao ya misitu nchini iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii mjini hapa juzi, Makani alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga katika kuhakikisha inaleta mabadiliko katika kila sekta.

Kutokana na mkakati huo mzito wa serikali, Makani aliwaomba watumishi wa idara ya misitu nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani hakuna atakaeendelea kuwalea.

“Watu wanashindwa kutofautisha kati ya uzoefu na mazoea," alisema Makani, kiasi kwamba "wanajikuta wanafanya kazi kama walivyozoea bila kuwaletea mabadiliko yoyote wananchi wanaowatumikia.
"Watumishi hao hawana nafasi katika serikali hii.”

Aidha, Makani alisema Rais John Magufuli ameonyesha mfano katika utendaji wake, hivyo watumishi hawana budi kumuiga na kuacha mazoea.

Akizungumzia uvunaji wa misitu nchini, Naibu Waziri huyo aliwataka wafanyabiashara wa zao hilo kujipanga katika kuhakikisha kuwa linakuwa endelevu tofauti na ilivyo hivi sasa katika baadhi ya maeneo kuharibiwa kabisa.

“Watu wanavuna misitu kwa wingi lakini hakuna jitihada za kuifanya misitu hiyo kuwa endelevu ili zao hili liendelea kuzalishwa kwa wingi na kuendelea kuliongezea kipato taifa letu," alisema Makani. "Mwisho wake mtavuna nini?”
Kwa mwaka heka 372,000 za misitu huwa zinaharibiwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama kilimo, ufugaji na uchomaji mikaa, alisema.

Naye Afisa Mtendaji mkuu wa TFS, Juma Mgoo, alisema kuwa ili kuweza kukabiliana na uhaba wa misitu wameweka utaratibu wa kupanda heka 8000 za miti kila mwaka.

Alisema kuwa mwaka jana walipanda heka 1,200 za miti katika maeneo mbalimbali lakini pia wamekuwa wakitoa elimu kwa wadau mbalimbali wa sekta ya misitu nchini ili kuweza kuzikabili changamoto za uharibifu wa misitu.

Habari Kubwa