Mitaala mipya elimu rasmi 2025

26Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Mitaala mipya elimu rasmi 2025

SERIKALI imesema mitaala mipya ya elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu inatarajiwa kuanza kutumika Januari mwaka 2025.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Aneth Komba, aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akiwasilisha mada ya mitaala na kupokea maoni ya wadau ya kuboresha mtaala huo.

Alisema kwa sasa kazi ya kukusanya maoni kwa wadau kwa ajili ya kufanya mapitio ya sita ya mitaala yanaendelea.

Hata hivyo, alisema mitaala inayotumika kwa sasa bado inafaa licha ya baadhi ya mambo yanaangaliwa kwenye mapitio ili yaongeze na yaendane na karne ya 21.

Kadhalika, Dk. Komba alisema ni vyema wasimamizi wa elimu kuhakikisha wanauelewa mtaala wa sasa kwa kuwa bado utaendelea kutumika hata baada ya kuanza kutumika mtaala mpya.

Wakitoa maoni yao kwenye mkutano huo, wadau hao walishauri masuala mbalimbali ikiwamo wahitimu wa darasa la saba waruhusiwe kuchagua kujiunga na elimu ya ufundi na siyo sekondari pekee.

Mratibu wa Elimu Dayosisi ya Arusha, Lushuru Sambwet, alishauri serikali kuangalia namna wanafunzi wanaohitimu darasa la saba kuwa na uchaguzi wa kujiunga na elimu ya ufundi na wengine kuendelea na sekondari.

Mkuu wa Shule Faraja maalum kwa watoto wenye ulemavu wa viungo, William Kivinyo, alishauri somo la lugha ya Kiingereza kuanza kufundishwa kuanzia elimu ya awali badala ya utaratibu wa sasa wa somo hilo kuanza kufundishwa kwa wanafunzi wa darasa la tatu.

Mwalimu wa Shule ya Lake Victoria, Juma Jackson, alishauri somo la stadi za kazi ambalo linafundishwa katika shule za msingi pekee lifundishwe pia kwa wanafunzi wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza na cha nne.

Habari Kubwa