'Mitandao ya kijamii itumike kutoa elimu kuikabili corona'

26Mar 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
'Mitandao ya kijamii itumike kutoa elimu kuikabili corona'

WADAU wamesisitiza kutumia mitandao ya kijamii, ikiwamo Facebook na WhatsApp, kutoa elimu ya kujikinga na maambukizo ya virusi corona nchini.

Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalotoa elimu kwa vijana kupitia michezo la YEs-Tz, Kenneth Simbaya, aliiambia Nipashe jana kuwa kuna haja mitandao hiyo itumike ipasavyo kusambaza elimu ya kujikinga na virusi hivyo hatari.

Alisema njia moja wapo ya kukabiliana na maambukizo ya ugonjwa huo ni kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook ambao una watumiaji wengi, kutoa elimu.

“Ni jukumu letu sote kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizo ya virusi vya corona kila mmoja kwa nafasi yake achukue tahadhari, mimi na shirika langu tutajikita kutoa elimu kupitia Facebook na imani watu wengi watasoma,” alisema.

Aliongeza kuwa shirika hilo lina lengo la kuwafikia vijana wengi mkoani Mbeya na katika kipindi hiki linawapa elimu ya uhusiano ili kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona.

Mratibu wa shirika hilo, Navina Mutabazi, alisema bado elimu inaendelea kuwafikia vijana kwa njia mbalimbali, ikiwamo kupiga simu kwa kushirikiana na wataalamu wa afya kwa kutumia mitandao ya kijamii.

"Taasisi yetu inaendelea kuwafikia vijana zaidi kuhakikisha elimu ya afya ya uzazi, masuala ya makuzi, wanapata kutoka kwa waelimishaji rika waliopo katika maeneo mbalimbali, elimu yetu inaanzia kwa vijana waliopo nje na waliopo shule," alisema.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya walipongeza hatua hiyo ya kutoa elimu ya maambukizo ya corona kwa kutumia mitandao ya kijamii, wakiamini itawafikia wengi.

Mmoja wa wakazi hao, Jesca Mwaipaja, alisema ni miongoni mwa wananchi watakaokuwa wanatembelea mtandao wa Facebook mara kwa mara ili kupata elimu ya kujikinga na virusi hivyo vinavyoisumbua dunia kwa sasa.

Habari Kubwa