Mitihani kidato cha sita kuanza Juni 29

23May 2020
Na Waandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Mitihani kidato cha sita kuanza Juni 29

SERIKALI imesema mitihani ya kidato cha sita nchini itaanza Juni 29 na kukamilika Julai 16, mwaka huu na itaenda sambamba na mitihani ya ualimu huku wanafunzi wakitakiwa kufika shuleni kwa wakati.

Pia, imewaagiza viongozi wa mikoa, wilaya na shule za kidato cha sita kuchukua tahadhari zote za afya ikiwamo kuhakikisha wanafunzi wote wanavaa barakoa na wa bweni kulala kwa umbali ili kujiepusha na maambukizo ya ugonjwa wa corona.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, alizitaka shule kufanya maandalizi ya kupokea wanafunzi hao Juni mosi, mwaka huu, huku akiwataka wa shule za bweni kuripoti Mei 30, mwaka huu.

Kuhusu tahadhari zitakazochukuliwa kwa wanafunzi wa bweni, kwa vitanda vya dabo deka, atatakiwa kulala mwanafunzi mmoja, bweni linalochukua wanafunzi 80, litatakiwa kuweka wanafunzi 40 na bweni lenye vitanda vilivyobanana, vitatakiwa kutenganishwa.

Kadhalika, aliagiza Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kusambaza ratiba ya mitihani hiyo mara moja, na kuhakikikisha matokeo yanatoka kabla ya Agosti 30, mwaka huu, ili wanafunzi watakaofanya vizuri wapate muda wa kutuma maombi vyuo vikuu bila kuathiriwa na muda.

Alisisitiza kuwa shule ambazo zinafunguliwa hivi sasa ni zenye wanafunzi wa kidato cha sita pekee.

“Kuhusu madarasa mengine utaratibu wao utaelekezwa baadaye, hivyo asije akatokeza mwanafunzi mwingine wa kidato cha kwanza au cha pili na vingine ambavyo havijaelekezwa kurejea shuleni,” alisema.

Kuhusu mikopo, Prof. Ndalichako alisema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Vyuo Vikuu tayari ina fedha kiasi cha Sh. bilioni 122.8 kwa ajili ya wanafunzi wenye sifa ya kupata mikopo hiyo.

“Kinachotakiwa ni vyuo kuwasilisha nyaraka muhimu na hadi Mei 28, mwaka huu, nyaraka hizo ziwe zimewasilishwa Bodi ya Mikopo ili itoe fedha hizo mara tu wanafunzi wanapofika vyuoni," alisema.

Aliviagiza vyuo kupitia mabaraza na Seneti kufanya maandalizi muhimu ili kufungulia kama alivyoagiza Rais John Magufuli.

Alivitaka vyuo kuhakikisha masomo yanaendeshwa katika mfumo ambao unafidia muda ambao wanafunzi wameupoteza kutokana na corona.

“Lazima ratiba zibadilike ili kuwa na muda zaidi wa kusoma kwa lengo la kufidia muda ambao umepotea na kwa vyuo vikuu na vya kati ziwasilishe utaratibu huo kwa mamlaka husika ambayo ni Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), ifikapo Mei 27, ili serikali ione kilichopangwa na kufahamu ratiba ya kila chuo na kujipanga kikamilifu kupitia bodi ya mikopo,” alisema.

Prof. Ndalichako alivitaka vyuo na shule kuchukua tahadhari ili wanafunzi wanaporudi wasije wakawa sababu ya kurudisha mlipuko wa ugonjwa huo.

“Vyuo na shule lazima viwe na sehemu za kunawia mikono hasa katika maeneo yanayoingiza wanafunzi wengi, madarasani, mabwalo na kumbi za mikutano na kuhakikisha utaratibu huo unatumika kikamilifu,” alisema.

Waziri huyo alisema serikali inaandaa mwongozo mahsusi kwa ajili ya vyuo na shule na amefanya mazungumzo na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, na kumwagiza Mganga Mkuu wa Serikali, kuandaa mwongozo huo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Mwita Waitara, alisisitiza shule kuhakikisha wanafunzi na walimu wanavaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka kwenye maeneo yote ya kuingilia shuleni na madarasani.

Aliagiza viongozi hao wa mikoa na wilaya kabla ya shule hizo kufunguliwa Juni mosi wakague na kuhakikisha mazingira rafiki yanakuwapo.

"Kuna uwezekano wazazi wakaingia gharama kidogo maana wanapaswa kuwanunulia barakoa lakini na watakaoweza kuwanunua vitakasa mikono ili kujikinga na ugonjwa wa Corona,"alisema.

Alisema walimu waandae wanafunzi kisaikolojia ili wafanye vizuri kwenye mitihani yao.

"Wanafunzi wanaweza kwenda na tangawizi na hata kujifukiza pia ruksa na wanafunzi wote lazima wapimwe joto, na wale wenye mahitaji maalum watakuwa na usimamizi mahususi na ikitokea dalili zozote tutachukua hatua,"alisema.

Alisisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kuripoti shule kwa muda uliopangwa na kutakuwa na adhabu za utoro kwa ambao hawataripoti kwa wakati.

“Kila siku tutakuwa tunapata taarifa na viongozi wa mikoa na wilaya wanawajibu wa kuzunguka kila siku,”alisema.

•Imeandikwa na Augusta Njoji na Renatha Msungu

Habari Kubwa