Mizigo bandarini Dar yaongezeka kwa 6.0%

09Oct 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Mizigo bandarini Dar yaongezeka kwa 6.0%

SHEHENA ya mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kutoka tani za uzito 16,197,818 mwaka 2017/18 hadi 17,166,079 mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.0.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko, alisema ongezeko hilo ni la tani 968,261 ikiwa ni kiwango cha juu kuwahi kufikiwa kati ya mwaka na mwaka katika historia ya mamlaka hiyo.

Alisema shehena ya kichele ambayo ni nafaka na bidhaa nyingine za aina hiyo ilipungua kwa wastani wa asilimia 2.7 kwa mwaka na kwa mwaka 2018/19 ilikuwa tani za uzito 2,191,697 ikilinganishwa na tani 1,896,748 za mwaka 2017/18.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, shehena ya kawaida kwa miaka mitano kuanzia 2014/16 hadi 2018/19 kulikuwa na ongezeko la shehena inayopakuliwa kutoka nje kwa asilimia 2.0.

Alisema kwa kipindi cha mwaka 2018/19 shehena ya kawaida iliyopakuliwa ilikuwa tani za uzito 5,681,419 ikilinganishwa na tani 5,224,330 za mwaka 2018/18 sawa na ongezeko la tani 457,088.

Alisema shehena ya kawaida ilikuwa ni tani 2,717,723 zikilinganishwa na tani za uzito 2,720,554 za mwaka 2017/18 sawa na upungufu wa tani za uzito 2,831.

Kakoko alisema shehena ya mafuta iliyohudumiwa kwa kipindi cha miaka mitano ilikuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 5.4 kwa mwaka.

Pia, shehena iliyohudumiwa kwa mwaka 2018/19 ilikuwa tani milioni 6.052 ikiwa ni ongezeko la tani 48,634 sawa na asilimia 0.8 ikilinganishwa na tani milioni 6.003 zilizohudumiwa mwaka 2017/18.

Kadhalika shehena ya makontena iliongezeka kwa asilimia 2.4 kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.0.

Kakoko alisema kwa kipindi cha miaka mitano mapato na matumizi yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 7.6 kwa mwaka, kiasi cha kupata ziada ya Sh. milioni 464.4, ikiwa ni pamoja na kuongeza kiasi cha fedha kinachopelekwa serikalini.

Alisema michango katika mfuko mkuu wa serikali iliongezeka kutoka Sh. bilioni 124.24 mwaka 2017/18 hadi Sh. bilioni 141.6 mwaka 2018/19.

Habari Kubwa