Mjema atoa msaada vifaa vya shule wanafunzi wanaoishi mazingira magumu

17Jan 2022
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Mjema atoa msaada vifaa vya shule wanafunzi wanaoishi mazingira magumu

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, ametoa msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akitoa msaada wa madaftari na kalamu kwa wanafunzi ambao wanaishi mazingira magumu katika shule ya Msingi Ushirika Manispaa ya Shinyanga.

Mjema ametoa msaada huo leo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya uandikishaji wanafunzi katika baadhi ya shule za msingi na Sekondari katika Manispaa ya Shinyanga.

Amesema serikali inatoa elimu bure, hivyo wanafunzi wote walioandikishwa kuanza shule, wanapaswa kuhudhulia masomo yao licha ya kutokuwa na sare za shule, na kuamua kutoa msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi ambao wanaishi katika mazingira magumu.

"Nimefarijika kuona hali ya uandikishaji wanafunzi siyo mbaya, naomba wazazi waendelee kuleta watoto wao shuleni, elimu ni bure na hakuna ulipaji wa ada,"

"Natoa agizo kwa Wakuu wa Shule na Walimu marufuku kurudisha wala kukataa kupokea wanafunzi ambao hawana sare za shule, wapokeeni waanze masomo, wakati wazazi wao wakiendelea kutafuta fedha za kuwanunulia vifaa vya shule," amesema Mjema.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amewataka wanafunzi wasome kwa bidii na kuacha utoro ili watimize ndoto zao, wakati serikali ikiendelea kuwaboreshea mazingira mazuri ya kusoma.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ushirika Manispaa ya Shinyanga Pendo Peter, amesema matarajio ya kuandikisha wanafunzi wa awali ni 75 lakini wameandikisha 43, darasa la kwanza matarajio 125 na wameandikisha 69.

Nao baadhi wanafunzi ambao wamepewa msaada huo, zikiwamo sare za shule, madaftari, na kalamu, wamempongeza Mkuu huyo wa Mkoa, huku wakiahidi kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao.

Habari Kubwa