Mkakati wa CCM kuchukua majimbo, ngome za upinzani

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mkakati wa CCM kuchukua majimbo, ngome za upinzani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kiliambulia majimbo manne kati ya 10 ya Mkoa wa Dar es Salaam katika Uchaguzi Mkuu uliopita, sita yakichukuliwa na wabunge kutoka vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Tayari chama tawala kimefanikiwa kuyarejesha majimbo mengine matatu ya Kinondoni, Ukonga na Temeke baada ya waliokuwa wabunge wake kujiuzulu uanachama wao kwenye vyama vya upinzani na kuhamia CCM ambako walipewa tena nafasi ya kuwania ubunge.

Wakati vyama mbalimbali vya siasa nchini vikijipanga kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, umezindua kampeni ya ‘Dar es Salaam ya Kijani’ yenye lengo la kuirudisha chama tawala mitaa na majimbo yaliyokwenda upinzani.

Kampeni hiyo inalenga kuweka mkakati kwa kuanzia ngazi za jumuiya zote za mkoa huo kujipanga kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Agosti, mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Chuo Kikuu Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, alisema wanaamini kampeni hiyo itachochea ustawi zaidi wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam.

“Leo (jana) tunazindua kampeni yetu ya Dar es Salaam ya Kijani kuelekea serikali za mitaa mwaka huu. Ni kampeni kabambe kwa ajili ya kuirejeshea CCM mitaa iliyopotea katika uchaguzi uliopita ambayo itatusaidia kupata ushindi mkubwa kimkoa katika Uchaguzi Mkuu mwakani kwenye udiwani, ubunge na urais.

“Sote ni mashuhuda kwamba katika uchaguzi uliopita wa 2014 wa Serikali za Mitaa na ule mkuu wa 2015, tulipoteza baadhi ya mitaa, kata na majimbo yaliyokuwa yakishikiliwa na CCM.

“Na sababu za kupoteza huko zinajulikana, sina haja ya kuzirejea sasa. Hivyo, sisi vijana wa CCM tunatambua kuwa ndiyo damu na roho ya chama chetu, na kwamba tunao wajibu wa asili wa kusafisha njia katika kutimiza malengo ya uwapo wa vyama vya siasa kikatiba ya kushika dola," Kilakala alisema.

Alisema CCM inahitaji ushindi mkubwa kwa kuweka mikakati ya awali kwa kuwahusisha wanachama wa chama hicho kwa ngazi zote.

“Kampeni yetu hii itashuka katika wilaya, kata na matawi yote katika mkoa wetu ili kuwa na ufahamu wa pamoja na kuhakikisha kila kijana wa UVCCM anawajibika ipasavyo kuhakikisha falsafa ya Dar es Salaam ya kijani, yaani Dar es Salaam ya CCM inaenea kwa wanachama na wananchi ili ikifika wakati wa uchaguzi, tuvune wapigakura wa kutosha," alisema.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Raymond Mwangwala, alisema ameridhishwa na kasi kubwa inayofanywa na vijana wa Dar es Salaam kuhakikisha chama kinapata heshima katika uchaguzi.

“Leo ninachokiona hapa, hii ndiyo UVCCM ninayoijua na sina shaka na uongozi wa mkoa kwa kuwa unafanya kazi kubwa na nzuri, ninachoweza kusema kwenu ninawaomba sana vijana tukilinde chama na kuhakikisha tunapata ushindi katika uchaguzi.

“Na ikiwezekana waachieni (upinzani) asimilia mbili tu ya mitaa na pindi ikibidi hata hakikisheni tunachukua asilimia zote 100. Vijana tushikamane na tulinde heshima ya chama chetu," Mwangwala alisema.

Habari Kubwa