Mkakati mpya Chadema uchaguzi 2020 waanikwa

25Jun 2018
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Mkakati mpya Chadema uchaguzi 2020 waanikwa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanika mkakati wake mpya wa kuongeza wanachama na kueneza sera zake kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Freeman Mbowe.

Kimesema mkakati huo unaohusisha uenezaji wa sera za kisiasa kuanzia ngazi ya familia, kimeanza kuufanyia kazi nchini kutokana na serikali ya awamu ya tano kupiga marufuku mikutano ya kisiasa hadi 2020, uchaguzi mkuu ujao. 

Katika mkutano wao na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, viongozi wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) walisema kuwa licha ya kuwapo kwa zuio hilo, chama kimeamua kuja na mbinu mpya za kufanya siasa, ili kiendelee kuvuna wanachama wapya na kunadi sera zake.

Makamu Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Hawa Mwaifunga, alisema baraza hilo ambalo limekuwa na mkutano wake wa mwaka kwa siku mbili kuanzia juzi jijini hapa, limeazimia kuwatumia wanawake kufanikisha mkakati huo mpya wa Chadema.

Mwaifunga alisema viongozi wa chama hicho sasa watakuwa wanafanya siasa kuanzia ngazi ya chini ya familia ili kuhakikisha zuio la mikutano ya kisiasa halikiathiri zaidi chama chao.

Alisema kuzuiwa kwa mikutano hiyo kumeminya demokrasia na kamatakamata ya viongozi wa upinzani iliyopo nchini imesababisha kina mama wengi kukosa nafasi na kuwaogopesha kufanya siasa majukwaani. 

“Tunajua kuwa serikali sasa imekuwa mstari wa mbele kukandamiza upinzani kwa kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa na kuwakamataviongozi wa upinzani. Mambo haya yanasababishwa na kuminywa kwa uhuruwa watu kujieleza na kutoa maoni yao," Mwaifunga alisema. 

“Kutokana na hali hiyo, baraza (Bawacha) tutafanya mafunzo kwa kinamama ili kuwajengea uwezo wa kujiamini, lakini ikumbukwe kuwa kwa sasa tumeanzisha mkakati mpya wa kufanya siasa kuanzia ngazi ya chini kabisa ya familia. 

“Tunayo majimbo sita ambayo yanaongozwa na wabunge wanawake wa Chadema. Mkakati wetu sasa ni kuhakikisha majimbo yetu hayachukuliwi na kuongeza mengine zaidi. 

“Tupo imara. Hata kama serikali imekuwa ikiwakamata viongozi wetu, wamezuia mikutano ya hadhara na kuna ukiukwaji  wa katiba, tutapambana na tutaendelea kufanya siasa na kutoa mafunzo kwa wanachama wanawake jinsi ya kufanya siasa mbadala na kuwajengea uwezo wa kujiamini ili kuhakikisha tunaongeza majimbo zaidi.” 

Majimbo sita yanayoongozwa na wabunge wanawake wa Chadema ni Kawe lililopo chini ya Halima Mdee, Mrimba (Susan Kiwanga), Bunda Mjini (Esther Bulaya), Tarime Mjini (Esther Matiko), Babati Mjini (Pauline Gekul) na Same Mashariki analoliongoza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka. 

BAJETI HEWA 

Mwaifunga pia alisema baraza hilo linaunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kwamba bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha ni 'hewa' na haitekelezeki kutokana na serikali kutokuwa na mipango yenye dira ya kumsaidia mwananchi wa kawaida.

Alisema wanaona serikali bado haijaweza kusaidia kukuza uchumi wa Mtanzania kutokana na matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa.

“Kutokana na hali hiyo, Bawacha tunaendelea kupiga kelele kwa ajili ya kudai Katiba mpya ili kujibu matakwa ya Watanzania sambamba na kutaka kuwapo kwa uhuru wa kufanya siasa, mihimili kuheshimiana sambamba na kuwapo uhuru wa kujieleza na kupata habari," alisema Mwaifunga.

Kiongozi huyo wa Chadema pia alisema baraza lao linaona kuna haja kuwa na mjadala wa wazi kuhusu hatima ya watoto wanaopata ujauzito wakiwa shuleni. 

Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace Tendega, alisema kwa sasa wanaendelea na mikakati mbalimbali ya muda mfupi na mrefukuhakikisha chama kinaendelea kuwa imara katika kipindi hiki alichodai ni ngumu kufanya siasa.

Mkutano huo wa Bawacha uliwahusisha makatibu wote wa baraza hilo, kutoka mikoa yote pamoja na viongozi wengine wa juu kwa lengo la kujadili hali ya kisiasa, uchumi na kujengeana uwezo wa kisiasa. 

 

Habari Kubwa