Mkandarasi wa Flashteck Ltd apewa siku 3 kukamilisha jengo la mil 700

26Sep 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe Jumapili
Mkandarasi wa Flashteck Ltd apewa siku 3 kukamilisha jengo la mil 700

MKUU wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amempa siku tatu, Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Flashteck Tanzania Limited, inayojenga maghala mawili ya kuhifadhia korosho katika eneo la Mtimbwilimbi katika Halmashauri ya Nanyamba wilayani Mtwara na Ndwika wilayani-

-Nanyumbu kuhakikisha anamaliza ujenzi wa majengo hayo kwa ajili ya kutumika kuanzia Oktoba mosi mwaka huu.

Brigedia Jenerali Gaguti, ametoa kauli hiyo leo mkoani humo, alipofanya ziara ya kukagua utayari wa kuanza kwa msimu mpya wa uuzaji korosho unaotarajiwa kufanyika Oktoba Mosi mwaka huu ambapo ametembelea baadhi ya mashamba ya wakulima katika eneo la Naliendele pamoja na ghala la Mtimbwilimbi.

Katika ziara hiyo Kaimu Meneja Mkuu wa  Chama Kikuu cha Ushirika cha Mtwara na Masasi (MAMCU) Biadia Mpika, amesema ujenzi wa maghala hayo ulianza Februari 20 mwaka jana na mpaka kufikia Julai mwaka huu yalikuwa yamegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.388 na kwamba ghala la Mtwimbwilimbi limevuka makadirio ya Ujenzi kwa mkandarasi kulipwa ziada ya shilingi milioni 80.

Akiwa katika eneo la Mtimbwilimbi kunakojengwa ghala hilo la kuhifadhia korosho Brigedia Jenerali Gaguti, amesema , mbali na kuhakikisha jengo hilo linakamilika ifikapo Jumatatu wiki ijayo, pia amemtaka kiongozi huyo wa mafundi kuwasilisha nyaraka zote za ujenzi wa ghala hilo katika ofisi yake kwa ajili ya ukaguzi na tathmini ya fedha zilizotumika.

"Mmeniambia hili ghala ni shilingi milioni 700 ninawataka muwasilishe nyaraka zenu ninyi kwa kushirikiana na Chama kikuu cha Ushirika cha Mtwara na Masasi (MAMCU), ili ofisi yangu ijiridhishe juu ya hizo gharama na hapa tutaangalia Item mojamoja na gharama zake haiwezekani jengo hili likatumia mwaka mzima kujengwa na bado halikamiliki" amesema Brigedia Generali Gaguti.

Amesema haikubaliki MAMCU wakaanza msimu wa uuzaji korosho kwa kukodisha ghala wakati tayari walishakopa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga maghala yatakayowasaidia kupunguza gharama za kuhifadhi korosho katika maghala ya watu binafsi.

Amewaagiza shirika la Umeme (Tanesco) Mkoa wa Mtwara kuhakikisha umeme unawaka katika jengo hilo kabla ya kuanza msimu mpya wa ununuzi wa korosho.

Akiwa katika eneo la Naliendele Brigedia Jenerali Gaguti, ametembelea Shamba la Korosho la Fakhi Hamis, ambapo mkulima huyo alimueleza kuwa msimu huu matarajio yake ni kupata magunia 50 tofauti na msimu uliopita ambapo alipata magunia 200.

Amesema walipuliza dawa katika muda muafaka wakiwa na matarajio ya kuvuka lengo lakini hali ya hewa imewaathiri kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na hali hiyo Brigedia Jenerali Gagut, amewataka wakulima hao kuhakikisha wanauza mazao yao katika vyama vya ushirika na kuepuka wanunuzi wa Kangomba kwa ajili ya kumuwezesha mkulima kufaidi matunda ya jasho lake.

Habari Kubwa