'Mkapa alifanikisha Msikiti wa Gaddafi'

01Aug 2020
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
'Mkapa alifanikisha Msikiti wa Gaddafi'

SHEIKH wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu, amesema atamkumbuka kwa mambo mengi mazuri Rais Benjamin Mkapa, ikiwa ni pamoja na namna alivyofanikisha ujenzi wa Msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma.

Akizungumza jana jijini Dodoma wakati wa ibada ya Eid El Hajj iliyofanyika katika msikiti huo, Sheikh Rajabu alisema Mkapa aliyezikwa Jumatano wilayani Masasi mkoani Kilimanaro, alikuwa kiongozi mwadilifu na msikivu kwa mkubwa na mdogo.

Sheikh Rajabu alisema alionana na Rais Mkapa Libya na kufanikisha ujenzi wa msikiti huo wa kisasa na atamkumbuka kiongozi huyo wa nchi kwa jambo hilo muhimu kwa waumini wa dini ya Kiislamu.

“Taifa limepata msiba mkubwa wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa. Pamoja na imani yake, amefanya mengi ambayo ni ya kukumbukwa, alikuwa muungwana sana," alisema.

Sheikh Rajabu alisema kuwa alikutana na Mkapa nchini humo miaka kadhaa iliyopita wakati huo yeye alikuwa akisoma na Rais Mkapa alifika kwa ajili ya kuiomba Serikali ya Libya kuwajengea Tanzania msikiti wa kisasa.

Alisema Mkapa alifika Libya akiwa na maombi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati huo, Mussa Nkangaa, kwa Serikali ya Libya wajengewe msikiti wenye hadhi.

“Tulikuwa vijana kadhaa ambao tulikuwa tukisoma kule Libya, tulienda mpaka katika hoteli ambayo alifikia, na tulikutana naye. Alishangaa kutukuta kule huku akisema yeye haelewi kitu kwani kila kitu kimeandikwa kiarabu.

“Alipoitwa kwamba tumefika, alishangaa kusikia kuna watanzania kule, lakini alishuka na tulizungumza naye kwa kirefu, hakika alikuwa ni muungwana, alipeleka ule ujumbe na Libya wakakubali kujenga msikiti huu ambao ndiyo tunaswali hapa," alisema.

Alisema wakati msikiti unakaribia kukamilika, Mkapa alifika na kukagua na hakuridhishwa na sehemu ya kunawia kwa kuwa ilikuwa juu, hivyo aliagiza ivunjwe.

“Hakuridhishwa na ile sehemu, akaagiza kuvunjwa, alisema mtu mfupi kama yeye atachukuaje udhu katika sehemu ambayo ipo juu vile, hivyo tulijenga kwa chini kidogo na sehemu za kukaa kwa kila mtu wakati akinawa," alisema.

“Mkapa alikuwa na mambo mengi sana, leo tunayaona na kusema sababu ameishafariki dunia. Mimi ninasema akiwa hai Rais wetu Magufuli ametupigania sana sisi Waislamu na ndiyo maana sasa unajengwa ule msikiti mkubwa jijini Dar es Salaam, anachapa kazi iliyotukuka."

CHUO KIKUU MOROGORO

Alisema jambo la pili ambalo analikumbuka kwa Mkapa ni kutoa jengo la umma la Shirika la Umeme (TANESCO) mkoani Morogoro na kuwapa waislamu ili kiwe Chuo Kikuu cha Kiislamu.

Alisema jambo hilo limeendelea kubaki katika kumbukumbu yake kwa kuwa Mkapa alikutana na wakati mgumu wakati watu walipohoji sababu ya kutoa mali ya umma kwa Waislamu.

“Kauli yake kwamba mali ya umma inatoa kwa wenye umma inaonyesha kwamba alikuwa muungwana sana na sisi waislamu tunapaswa kuendelea kumwombea kwani hata vitabu vitakatifu vinatutaka kuwaombea kwa mazuri marehemu wetu,” alisema.

Habari Kubwa