Mke, mume kortini kwa dawa za kulevya

06Dec 2017
Hellen Mwango
Nipashe
Mke, mume kortini kwa dawa za kulevya

WATU watatu, wakiwamo wanaodaiwa kuwa mume na mke, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 375.20.

Washtakiwa hao ni Minda Mfamai, Fatuma Mpondi na Oswin Mango, walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri.

Wakili wa Serikali, Adolf Nkini, alidai kuwa Novemba 22, mwaka huu, eneo la Chamazi kwa Mkongo, Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya.

Hakimu Mashauri alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu.

"Kwa kuwa washtakiwa mnakabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi, mahakama yangu haina mamlaka ya kusikiliza hadi upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu au Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP)  atakapowasilisha kibali cha kusikilizwa hapa, " alisema Hakimu Mashauri.

Hata hivyo, mshtakiwa Mfamai aliomba kibali cha kuzungumza mahakamani akiomba mahakama kuuamuru upande wa Jamhuri kumpeleka hospitali kutibiwa kwa kuwa amepata kipigo akiwa kituo cha polisi.

"Upande wa Jamhuri mhakikishe mshtakiwa anapatiwa matibabu kama alivyoomba. Kesi hii itatajwa Desemba 19, mwaka huu," alisema hakimu baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Habari Kubwa