Mke wa Dk. Salim afariki dunia

21Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mke wa Dk. Salim afariki dunia

RAIS John Magufuli ametuma salamu za pole kwa familia ya Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, kwa kumpoteza mke wake, Amne Rifai.

Jana, akiwa Mjini Same mkoani Kilmanjaro, Rais Magufuli aliwaomba wananchi waliokuwa katika mkutano wake wa kampeni za uchaguzi mkuu kusimama kwa dakika moja kumwombea kwa Mungu, Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Dk.  Salim Ahmed Salim, aliyefariki ghafla asubuhi ya jana.

“Pia tuendelee kumwombea ndugu yetu Salim ambaye bado anaumwa ili Mungu akamponye. Roho ya marehemu mke wa Dk. Salim ipumzike kwa amani na afya ya Dk. Salim ambaye ameugua kwa muda mrefu sasa na hawezi kutembea nayo ikaimarike na ikaponywe na Mwenyezi Mungu. Amin.”

Dk. Salim mwenye umri wa 78, alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Aprili 24, mwaka 1984 hadi Novemba 5, mwaka 1985, amewahi kuhudumu kama mwanadiplomasia nguli katika Umoja wa Mataifa (UN).

Pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

Kiongozi huyo ameshapata nishani mbalimbali za nyota ya Afrika, nishani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nishani ya kitaifa ya Vilima Elfu Moja, nishani ya kipendo (Msalaba Tukufu), ya Sifa (Ofisa Tukufu), Medali ya Afrika, Nishati ya Kitaifa cha Simba (Ofisa Tukufu).

Aidha, alipata nishani ya Miti Miwili ya Naili, nishani ya El-Athir, nishani ya Mono, Masahaba wa O.R. Tambo (Dhahabu), nishani ya Mwenge (daraja la pili).

Aidha, alipata tuzo za heshima kutoka vyuo vikuu mbalimbali za udaktari wa sheria mara mbili, Humanities, Sheria ya Kiraia, Sanaa katika masuala ya Kimataifa na Falsafa katika Uhusiano wa Kimataifa.

Habari Kubwa