M'kiti Chadema awekwa pembeni

17Apr 2018
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
M'kiti Chadema awekwa pembeni

BARAZA la Uongozi la Mkoa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo limemsimamisha Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Morogoro, James Mkude kwa tuhuma kadhaa ikiwemo madai ya utapeli mkoani Kilimanjaro.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Morogoro, James Mkude.

Kufuatia kusimamishwa kwa Mkude, nafasi yake itabaki wazi kabla ya kuteuliwa kaimu, imeelezwa.

Mwenyekiti huyo kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kujipatia Sh. milioni 400 kwa njia ya udanganyifu.

Akitangaza maamuzi ya baraza hilo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Suzan Kiwanga alisema maamuzi ya kumsimamisha yametokana na kujiridhisha na kufuata katiba katika kipengele cha maadili ambacho kinamkosesha sifa kiongozi anayetuhumiwa kwa jinai.

“Tunapenda kuwatangazia umma pamoja na wanachama na wapenzi wa Chadema kuwa kuanzia leo tumemsimamisha rasmi Ndugu James Mkude kwa tuhuma anazotuhumiwa," alisema Kiwanga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mlimba.

Mwenyekiti huyo alisema Chadema haikufurahishwa na tuhuma binafsi zinazomkabili mwenyekiti huyo hivyo imeona ni bora wamuweke pembeni ili kumaliza tatizo lake na kwamba hajafukuzwa kwenye chama hicho.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,  Ulrich Matei, Mkude anatuhumiwa kujipatia Sh. milioni 500 kutoka kwa Rose Temba, mkazi wa Majengo mjini Moshi baada ya kujifanya mganga wa kienyeji.

Alimdanganya pia Temba kuwa ana uwezo wa kurudisha uhai wa mtoto wake Baraka Temba aliyefariki kwa ajali ya gari mwaka jana, imedaiwa. 

Kiongozi huyo wa Chadema na mfanyabiashara mkoani hapa anadaiwa kumwambia mama huyo kuwa yeye ni mganga wa kienyeji na kumuhakikishia kwamba mtoto wake hakufa ajalini bali alichukuliwa kichawi.

Licha ya Temba kutoa Sh. milioni 400 kati ya fedha walizokubaliana, Mkude hakuweza kumrudisha mtoto huyo. 

Kamanda Matei alisema baada ya kumhoji wamebaini mtuhumiwa huyo alishirikiana na wenzake na kwamba wametengeneza mtandao ambapo wamekuwa wakifanya matukio hayo ya utapeli kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kamanda Matei alisema mtuhumiwa huyo alisafirishwa kuelelea Jijini Dar es Salaam kuonyesha wenzake anaofanya nao utapeli na baadaye atapelekwa mkoani Kilimanjaro kujibu mashitaka mahakamani.

Habari Kubwa