Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhandisi Emmanuel Kalobelo, alisema hayo mjini Morogoro mbele ya Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, kuhusiana na sekta ya uchumi na uzalishaji mali kupitia kilimo.
Kalobelo alisema mkoa huo una jumla ya mashamba makubwa sita yenye ukubwa wa hekta 19,834 kati ya eneo hilo linalolimwa ni hekta 7,573, na wakulima wadogo 14 wenye mashamba yenye ukubwa wa hekta 245.
Alisema zao la mkonge lilikuwa linalimwa katika halmashauri za Kilosa na Morogoro, lakini kutokana na uhamasishaji uliofanyika na viongozi, kwa sasa halmashauri za Gairo na Mvomero nazo zimeanza kulilima.
Alisema katika kuendeleza zao hilo, Halmashauri za Gairo na Morogoro zimeanzisha vitalu vya miche 32,000.
“Tumeanza shughuli za uhamasishaji na kufanya mafunzo ya kilimo cha zao la mkonge kwa wataalamu wa kilimo 83 na wakulima 104, na uzalishaji wa vitalu vya miche ya mkonge umefanyika,” alisema Kalobelo.
Alisema mkoa umeamua kuwapanga maofisa ugani katika maeneo yanayolimwa mkonge ili wakulima wapate ushauri wa kilimo na hatimaye wazalishe kwa tija.