Mkulima adaiwa kuuawa kwenye mgogoro na wafugaji

05Jan 2017
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Mkulima adaiwa kuuawa kwenye mgogoro na wafugaji

WIKI moja baada ya mkulima wa kitongoji cha Upangwani, Kijiji cha Dodoma Isanga, wilayani Kilosa, kuchomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni na wafugaji, migogoro ya wakulima na wafugaji imeendelea kuwa tishio na kuhamia Wilaya ya Morogoro na kusababisha kifo cha mkulima mmoja.

Mkulima huyo, Fabian Bago (21), amefariki dunia katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kukatwa mapanga kichwani na watu wanaodaiwa kuwa ni wafugaji wa jamii ya Kisukuma.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank Jacob, akithibitisha kifo cha mkulima huyo, alisema kijana huyo alifariki dunia majira ya saa 11 jioni juzi, akiwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali hiyo ukisubiri taratibu zingine za kipolisi.

Alisema, mara baada ya kufikishwa hospitalini akitokea Kijiji cha Kolelo, Wilaya ya Morogoro, alifanyiwa vipimo na matibabu, lakini alifariki dunia kutokana na kupata majeraha katika sehemu ya ubongo.

Baba mzazi wa kijana huyo, Alan Bago, alisema ameshatoa taarifa polisi kuhusu kifo hicho, anachosubiri ni maelekezo ya polisi ili aweze kuendelea na taratibu za mazishi.

Alisema, kifo cha kijana wake kimeathiri familia hiyo kutokana na kuacha mke na mtoto mmoja huku yeye akiwa hana uwezo wa kuihudumia familia hiyo iliyoachwa na marehemu.

Alisema matukio ya kupigwa na kuuawa yanayotokana na migogoro ya wakulima na wafugaji, yanasababisha kuwapo kwa wajane, yatima na walemavu hivyo lazima serikali ichukue hatua kukabiliana na migogoro hiyo.

Tukio la kujeruhiwa kwa kijana huyo lilitokea Januari mosi, majira ya saa saba katika kijiji cha Kolelo, wakati akiwa na rafiki yake walivamiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafugaji wa jamii ya Kisukuma na kukatwa mapanga kichwani.

Rafiki wa marehenu anaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha afya Duthumi.

Habari Kubwa