Mkurugenzi awaonya wezi wa maji ili kutumiza lengo 95% 2020

06Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mkurugenzi awaonya wezi wa maji ili kutumiza lengo 95% 2020

Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Rosemary Lyamuya amewataka wenye tabia ya kuchepusha mita za maji kuacha mara moja kwani kwa kufanya hivyo kunakwamisha malengo ya kufikisha huduma ya maji Dar es Salaam kwa asilimia 95 ifikapo 2020.

Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani, dawasa Rosemary Lyamuya.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati alipotembelea banda la DAWASA katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya 43 maarufu Saba Saba.

"Kama kuna wateja ambao wanatumia maji bila kutumia mita wanatakiwa kuja DAWASA kusajiliwa lakini pia kwa wale wanaochepusha mita za maji kuacha tabia hiyo mara moja kwani kwa kufanya hivyo wanakuwa wanahujumu shirika letu na tunashidwa kufikia malengo yetu ya kufikisha huduma za maji kwa asilimia 95 ifikapo 2020," amesema

Bi Rosemary amesema moja ya kazi ya Idara yake ni kukagua miradi mbalimbali ya Majisafi na Majitaka pamoja na kuhakikisha miradi ambayo inakaguliwa inaendana na mikataba ambayo ambayo ipo ndani ya Bajeti.

Ameongeza kuwa kwa upande wa mikataba sita iliyosainiwa hivi karibuni wataakikisha inafanyiwa ukaguzi na iendane na mikataba iliyosainiwa na kuhakikisha wakandarasi wanafuata mikataba kama inavyosema.

"Katika kitengo chetu tumekuwa tukikagua miradi mbalimbali pamoja na miundombinu na pale tunapokuta hitilafu tunaifanyia kazi. Niombe rai kwa wakazi wa Dar es Salaam, Kibaha na Bagamoyo kutoa taarifa pale watakapokuta miundombinu ina hujumiwa kwa kupiga simu kitengo cha huduma kwa wateja," amesema

Habari Kubwa