Mkurugenzi CDA kortini matumizi ya madaraka

12May 2018
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Mkurugenzi CDA kortini matumizi ya madaraka

WATU wawili akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Paskas Muragili, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Paskas Muragili.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Joseph Fovo, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa  (Takukuru), Biswaro Biswaro, alidai kuwa Muragili na Lemanya Benjamini, ambaye alikuwa Fundi sanifu wa mamlaka hiyo, walitenda kosa hilo Septemba, 2016.

 

Biswaro alidai kuwa washtakiwa hao hawakuweka wazi maslahi yao kuhusiana na ombi la kampuni ya Glaciaer Investment Co.Ltd kwenye zabuni Na. LGA/020/2016-2017/W/09 yenye thamani ya Sh. milioni 86.1 kuhusiana na ukarabati na ujenzi wa makaravati katika barabara za jiji la Dodoma.

 

Alisema watu hao walifanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007.

 

“Kitendo hiki ni ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi wa umma, Namba 7 ya mwaka 2011,” alidai .

 

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Fovo aliwahoji washtakiwa ambapo walikana mashtaka hayo.

 

Hakimu Fovo aliwapa masharti ya dhamana ambayo ni kila mmoja kuweka fedha taslimu Sh. milioni 23 au mali isiyohamishika pamoja na kuwasilisha hati za kusafiria. Washtakiwa walitimiza mashatri hayo na watakuwa nje lakini hawaruhusiwi kusafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama.

 

Fovo alisema Kesi hiyo itapangwa kusikiliza hoja za awali Juni 4, mwaka huu.