Mkurugenzi Dangote amshangaza Muhongo

31Oct 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Mkurugenzi Dangote amshangaza Muhongo

SERIKALI imeushauri uongozi wa kiwanda cha saruji cha Dangote kufuata sheria, taratibu na makubaliano baina ya kamati ya wazalishaji na watumiaji wa makaa ya mawe nchini.

Ushauri huo umetolewa kufuatia malalamiko ya Mkurugenzi Mkuu wa Dangote, Harpreet Duggal kwamba kiwanda chake kinalazimika kutumia fedha nyingi kujiendesha kutokana na pamoja sababu nyingine, kuzuiwa kuingiza makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini kwa bei rahisi.

Duggal alidai serikali imetaka kiwanda hicho kitumie makaa ya mawe ya kutoka mgodi wa Liganga ambayo ni ya kiwango cha chini na yanauzwa kwa bei ya juu pia.

Dangote pia ililalamikia kuuziwa gesi asilia kwa bei ya juu, kama Dar es Salaam, wakati nishati hiyo inatoka karibu na kiwanda kuliko wateja wa mkoa huo.

Lakini akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu kuhusu madai hayo jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema malalamiko ya mwekezaji huyo hayana ukweli na ni uzushi.

Muhongo alimtaka mwandishi wa Nipashe kumuuliza Duggal maswali matatu:

"Je, tumewahi kuwa na kikao cha wazalishaji na watumiaji wa makaa ya mawe ya Tanzania? Je, mlikubaliana na kuweka kamati ya kufuatilia matatizo yenu (watumiaji)? Umeshaenda kwenye kamati kulalamikia bei na ubora wa mkaa?"

Muhogo alisema anachoona ni kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Dangote "anakwepa uhalisia ulio kwenye makubaliano ya wazalishaji na watumiaji".

“Watumiaji nao wamo kwenye kamati mbona hilo haliongelei?

"Atujibu maswali."

WAziri huyo pia alitaka Dangote aulizwe "walivyokaa kikao na TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) kuhusiana na suala la gesi, walikubaliana nini?”

Waziri huyo alisema inashangaza kama wanakaa na kukubaliana, halafu mwekezaji huyo anakimbilia kwenye vyombo vya habari kulalamika.

“Kinachoonekana ni uzushi na ubabaishaji wa watu ambao wana maslahi yao ya kuagiza hivyo vitu na hatujui wanapata nini.”
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Kapuulya Musomba, alisema shirika lake linauza gesi kwa sheria na taratibu zilizopo na kwamba bei elekezi inapangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura).

“Inapotokea mtu anataka auziwe juu au chini ya ile iliyopangwa na Ewura, hatuna mamlaka ya kubadilisha," alisema Musomba.

"Mtu anaweza kuongea lolote kwa sababu sisi ndiyo tunahusika na gesi lakini tunafuata taratibu kwa kupeleka maombi kwa Ewura, unatuambia kwa jinsi ulivyoleta maombi yako na utauza bei hii. Hapo ndipo tuliposhindwana na Dangote.”

Alisema bei iliyopo kwa sasa ni dola za Marekani 5.12 kwa kila ‘MMBTU’.

Kuna wakati Dangote alitaka kuuziwa kwa dola 4.75, alisema Musomba, lakini baadaye aliandika barua kuwa hataki bei hiyo, anataka chini ya dola nne. "Ewura ilishindwa kumtimizia".

Alisema wiki tatu zilizopita walipokea barua kutoka kwa Dangote wakitaka TPDC ihakikishe wanapata umeme wa megawati 25 ifikapo Februari mwakani, na kwamba walikutana nao na kukubaliana kuzalisha umeme wa gesi kwa kiwango hicho kwa kampuni ambayo wameiidhinisha.

“Kuna tofauti kubwa kati ya gesi inayotokana na mafuta ambayo baada ya kutolewa mafuta ni uchafu na gesi asilia," alisema.
"Nigeria gesi ni mabaki ambayo wanaweza kuichoma au kutoa bure kwa kuwa wamerudisha gharama zao kwa kutumia mafuta.”
Mmiliki wa kiwanda cha saruji cha Dangote ni Aliko Dangote, mfanyabiashara tajiri zaidi barani Afrika.

Alisema iwapo TPDC itauza gesi kwa bei anayotaka Dangote, hakutakuwa na faida kutokana na mwekezaji huyo kulinganisha gesi ya Tanzania na ya kwao (Nigeria) ambako gesi ni bidhaa ya pili inayopatikana baada ya kutoa mafuta na uamuzi wa kuichoma au kuigawa bure huwa ni uamuzi kwa mujibu wa sheria za nchi husika.

“Nimeshakwenda kiwandani kwake, anasema kwa mwezi anapoteza dola za Marekani milioni tatu kwa kutumia mafuta, ukipiga hesabu ya matumizi ya mafuta na gesi kwa bei yetu, matumizi ya gesi yako chini sana. Tunachofanya ni haki na kwa wema, tunawapenda wawekezaji lakini ni lazima tukubaliane mambo ya msingi,” alifafanua.

Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda, alisema wamesikia malalamiko hayo hivi karibuni na kwamba hakukua na mawasiliano mazuri baina ya uongozi wa kiwanda na mkoa.

Alisema kwa sasa wako kwenye hatua nzuri iliyofikiwa na TPDC katika kusaka makubaliano ya kinachotakiwa kutumika kwa sasa kati ya gesi na mafuta.

Mkurugenzi huyo wa Dangote alida hutumia lita laki mbili za mafuta ya dizeli kila siku kuzalisha saruji katika kiwanda hicho kikubwa zaidi Afrika Mashariki kwa bidhaa hiyo.