Mkurugenzi Hal. Songea naye `atumbuliwa jipu'

26Feb 2016
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe
Mkurugenzi Hal. Songea naye `atumbuliwa jipu'

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Sixbert Kaijage, amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo na kuisababishia serikali hasara kubwa kutokana na miradi mingi kutokamilika na kujengwa chini ya kiwango.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Benson Mpesya.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Benson Mpesya, alisema Kaijage alikwenda kumuaga ofisini kwake na kumueleza kuwa amepewa barua kutoka wizarani ya kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi kuanzia Februari 24, mwaka huu.

Mpesya alisema kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, mtumishi akibainika kufanya ubadhirifu, anasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika.

Alisema kama atabainika kuwa amehusika na tuhuma zinazomkabili, atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

Baadhi ya madiwani ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walisema katika vikao vya Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo, walibaini kuwapo kwa ubadhirifu wa fedha katika miradi ya maji, barabara na majengo kwamba miradi iliyojengwa ipo chini ya kiwango.

Hivi karibuni, Baraza la Madiani la Halmahauri ya Wilaya ya Songea liliwasimamisha na kuwafukuza kazi Mhandisi wa Maji, John Undili na Mhandisi wa Barabara, Daud Basilio na kufanya idadi ya wakuu wa idara waliosimamishwa kufikia wanne.

Habari Kubwa