Mkurugenzi Nanyamba akalia kuti kavu

11Feb 2024
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Mkurugenzi Nanyamba akalia kuti kavu

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara, Thomas Mwailafu amekataliwa na Madiwani kwa madai kuwa hana ushirikiano na ana hatarisha kura zao kwenye uchaguzi Mkuu 2025.

Uamuzi wa Madiwani hao umefikiwa leo baada ya Baraza lao kujigeuza kuwa kamati kumjadili Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo ambaye hakuwepo kikaoni alipotafutwa amejibu kuwa atakaporejea atatoa maelezo licha ya kutosikia malalamiko juu yake.

Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Jamal Kapende, amesema wamejadili mambo matatu ikiwamo utendaji kazi wa Mkurugenzi ambapo  Madiwani wametoka na kauli ya kumkataa kwa madai kuwa hana ushirikiano na kupuuza ushauri wao.

"Utendaji wake ni kikwazo kwa madiwani wanachokiona ni kwenda kufeli 2025 kwa kuwa wananchi watakuwa hawayaoni matokeo, niwaombe watendaji wa Halmashauri kila mtu acheze kwa namba yake atoe pasi, lawama ziwe kwa mfungaji,"amesema.

Awali, kabla ya kufikia uamuzi huo, Diwani wa Kata ya Nanyamba, Hassan Mauji, amesema wanataka kujadili utendaji wa Mkurugenzi na mahusiano na watumishi wa Halmashauri hiyo lakini anazuia na kumuomba Katibu Mkuu Tamisemi kumuondoa Mkurugenzi.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Wakili Prosper Kisinini, amesema suala la baraza kujigeuza kuwa kamati ni kinyume na taratibu na Mkurugenzi huyo yupo chini ya mamlaka ya Katibu Mkuu.