Mkurugenzi, TFS mikononi mwa Takukuru

20May 2020
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Mkurugenzi, TFS mikononi mwa Takukuru

​​​​​​​MKUU wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Salehe Mhando, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuichunguza ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na ofisi ya Wakala wa Misitu(TFS) kwa kuhusishwa na tuhuma za-

Magunia ya mkaa yaliyo taifishwa.

-kutoa vibali vya uvunaji miti bila utaratibu.

Mhando ametoa agizo hilo jana katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha wilaya hiyo baada ya kufanya msako wa kushtukiza katika mapori na misitu mbalimbali wilayani humo ambapo alibaini kuwepo kwa uvamizi na uvunaji misitu holela katika mapori mbalimbali.

Mhando amekamata zaidi ya magunia 7,000 ya mkaa katika pori la Bulamata wilayani humo ambapo wahusika walitaka kutorosha nje ya Wilaya hiyo.

Baada ya kukamata magunia hayo, ameamuru mkaa huo kutaifishwa kwa alichoeleza kuwa hauna vibali vya uvunaji na yeye kama sehemu ya watia saini za vibali vya uvunaji rasilimali za misitu katika wilaya hiyo hana taarifa yoyote.

Meneja wa TFS wa Kanda ya Magharibi inayojumuisha Mkoa wa Katavi, Kigoma, Shinyanga, Tabora, Valentin Msusa, amesema wamejipanga kudhibiti vitendo vya uvunaji holela wa bidhaa za misitu.

Amesema wao kama wasimamizi na walinzi wa rasilimali za misitu wanahakikisha hakuna mtu anayefanya biashara ya mkaa, mbao na bidhaa yoyote ya msitu kwa kuvunja sheria za misitu.

Hata hivyo, Msusa amesema tukio hilo ni fundisho kwa wengine wasiofuata sheria na baadhi ya watumishi wa TFS wanaoshindwa kusimamia majukumu yao.

Habari Kubwa