Mkurugenzi wa jiji Mwanza anusurika kupigwa na wamachinga

08Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mkurugenzi wa jiji Mwanza anusurika kupigwa na wamachinga

MKURUGENZI wa jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amenusurika kupigwa na wafanyabiashara wadogowadogo maarufu wamachinga wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara ya Pamba na mtaa wa Sokoni jijini humo.

MKURUGENZI wa jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba.

Tafrani hiyo imezuka  baada ya Mkurugenzi huyo kutoa maelezo kwa wafanyabiashara hao wanaotakiwa kupisha maeneo hayo na kuhamia kwenye soko la muda eneo la Kata ya Mbugani. 

Mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa Machinga mkoani Mwanza Mahida Suleiman amesema tayari maeneo yote yamejaa wafanyabiashara wadogo, huku Bi. Anastazia Wambura ambaye ni mjasiriamali  akiziomba mamlaka kuheshimu  maelekezo ya rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ya kutowabugudhi  machinga.

Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba amesema timu ya wataalam 6 kutoka jiji itapita kwenye maeneo yao kwa ajili ya kuwasajili ili wapangiwe maeneo ya soko la muda kata ya Mbugani.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella akizungumza katika kikao cha bodi ya barabara cha robo ya kwanza kwa mwaka 2019/2020, alimuagiza mkurugenzi wa jiji la mwanza pamoja na mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela, kuona namna bora ya kuwapanga wafanyabiashara wadogo waliopo pembezoni mwa barabara kuu ya Mwanza - Musoma na za mitaa ya katikati ya jiji hilo ili wasiendelee kuzagaa ovyo barabarani.

Soma zaidi: https://www.ippmedia.com/sw/biashara/machinga-wagoma-kuhama-mwanza

Habari Kubwa