Mkurugenzi wa shule mbaroni madai kujeruhi

19May 2022
Francis Godwin
IRINGA
Nipashe
Mkurugenzi wa shule mbaroni madai kujeruhi

JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia Mkurugenzi wa Shule ya Sun Academy, Nguvu Chengula (50), kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kitako cha bastola mzazi aliyekwenda shuleni huko kuomba kuhamisha mtoto wake kwenda shule nyingine.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, aliwaambia wanahabari jana kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa sita mchana Mei 16, mwaka huu, katika eneo la Shule ya Sun Academy iliyoko Mawelewele mjini Iringa.

Kamanda Bukumbi alidai Chengula alimjeruhi Alifa Mkwawa, maarufu Wilbert (35), mjasiriamali mkazi wa Isakalilo mjini Iringa kwa kutumia kitako cha bastola yake aina ya Cabin 55 yenye namba za usajili 6472-15100082 anayomiliki kihalali na kumsababishia jeraha sehemu ya kichwani.

"Hatua hiyo ilijitokeza baada ya mlalamikaji kwenda shuleni hapo na mwenza wake Prisca Kimaro (30), mjasiriamali wa Isakalilo, kwa nia ya kuomba uhamisho wa mtoto wao (6) anayesoma darasa la pili shuleni hapo," alidai.

Alisema kuwa chanzo cha mzozo ni mtuhumiwa kugoma kutoa uhamisho wa mwanafunzi ambaye ni mtoto wa mlalamikaji.

Alisema mtuhumiwa amekamatwa pamoja na kielelezi cha bastola ambayo imehifadhiwa kituoni na pindi upelelezi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani.

Habari Kubwa