Mkurugenzi wa zamani wa IPP afariki dunia

16Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mkurugenzi wa zamani wa IPP afariki dunia

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Mipango wa IPP Limited, Francis Zangira, amefariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Makao Makuu ya IPP, Zangira alifariki dunia jana, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa hiyo ilisema mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwa marehemu mtaa wa Isebi nyumba namba 21, Mbezi Tangi Bovu, jijini Dar es Salaam.

Mtoto wa kwanza wa marehemu, Steven Zangira, alisema bado walikuwa hawajakaa kama familia ili kujua siku ya mazishi na wapi yatakakofanyika.

“Msiba umetokea muda si mrefu, hivyo tunasubiriana ndugu tukae leo jioni (jana) tutapanga na kuwataarifu kuhusu kitakachoendelea,” alisema.

Steven alisema baba yake aliugua ghafla juzi akiwa ofisini kwake na kupelekwa Hospitali ya Hindumandal.

Hata hivyo, alisema hali yake ilizidi kuwa mbaya na alihamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi na kufariki dunia jana saa 5:00 asubuhi.