Mkutano Baraza la Mawaziri Sadc waanza

28May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mkutano Baraza la Mawaziri Sadc waanza

MKUTANO wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) umefanyika jana kwa njia ya mtandao, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

Mkutano huo ulifunguliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Maofisa Waandamizi/Makatibu Wakuu, Balozi Kanali Wilbert Ibuge, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wajumbe wengine waliohudhuria ni Katibu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzuki, pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipago, Amina Shaaban.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri utafanyika kesho baada ya kukamilika kwa kikao cha kamati hiyo ambayo imejadili masuala mbalimbali ndani ya jumuiya ikiwamo mlipuko wa virusi vya corona ndani ya SADC.

Mkutano huo utaangalia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri kilichofanyika mwezi Aprili 2020 kuhusu Covid-19 na athari zake katika utekelezaji wa programu za SADC, athari za kijamii na kiuchumi na madhara yake ndani ya jumuiya.

Pia, mkutano huo umejadili hali ya kifedha ndani ya jumuiya, utekelezaji wa maazimio yaliyotokana na kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC ambayo ni Menejimenti ya Maafa, utekelezaji wa kaulimbiu ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC isemayo "Mazingira Wezeshi kwa ajili ya Maendeleo Endelevu na Jumuishi ya Viwanda, Kukuza Biashara na Ajira ndani ya SADC" na mapitio ya hali halisi ya biashara baina ya nchi, maendeleo ya viwanda ndani ya jumuiya na taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa Jumuiya na Mpango kazi wake.

Mkutano huo umehusisha wataalamu kutoka nchi wanachama 12 wa SADC sekta za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha na Mipango, Uchukuzi na Mawasiliano, Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii pamoja na Afya.

Habari Kubwa