Mkutano mkuu CCM ulivyoacha maswali

11Dec 2022
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Mkutano mkuu CCM ulivyoacha maswali

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wiki hii kilifanya Mkutano Mkuu wa Taifa wa 10 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma. Mkutano huo uliofanyika Desemba 7 na 8 chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, ulikuwa wa kikatiba na hufanyika kila baada ya miaka mitano.

Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkutano Mkuu huo ambao pamoja na mambo mengine uliwachagua mwenyekiti wa taifa, makamu wenyeviti bara na Zanzibar na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka makundi ya wanawake na wanaume pande zote.

Rais Samia alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM huku Abdulrahman Kinana akiendelea kuaminiwa katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyetiki Zanzibar.

Licha ya viongozi hao wakuu wa chama kuchaguliwa, mkutano huo mkuu umeacha maswali mengi ambayo yanashindwa kutoa majawabu ya moja kwa moja huku wateule ndani ya chama na serikali wakiwekwa njiapanda kuhusu uhakika wa kuendelea kutumika katika nafasi walizo nazo.

KIPORO MABADILIKO

Kama ilivyo ada unapofanyika mkutano mkuu wa Taifa,  mabadiliko makubwa hutarajiwa hasa katika sekretarieti kwa maana ya Katibu Mkuu na naibu makatibu wakuu wa Bara na Zanzibar,  wakuu wa idara za fedha na uchumi, itikadi na uenezi, organaizesheni, na siasa na uhusiano wa kimataifa.

Tofauti na ilivyozoeleka, mabadiliko ya sekretarieti hiyo yamewekwa kiporo huku ikiahidiwa kuwa yatafanyika siku chache zijazo. Sekretarieti hiyo huteuliwa na NEC, hivyo majaliwa ya vigogo walioko katika nafasi hizo yako mikononi mwa wajumbe wa chombo hicho ambacho ni kama bunge la chama.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe wa sekretarieti, wakiongozwa na Katibu Mkuu, Daniel Chongolo, presha inapanda, mara inashuka kwa kuwa hawaelewi mustakabali wao kama wataendelea au la.  Miongoni mwao waligombea ujumbe wa NEC huku baadhi wakipeta na wengine kuangukia pua.

SERIKALI KUFUMULIWA

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM,  Rais Samia, aliomba wajumbe wa Mkutano Mkuu wampe ridhaa ya kuifumua serikali yake kwa kile alichoeleza kuwa kuna baadhi ya wateule wake hawaendani na kasi yake.

Hali hiyo inazua maswali ni mabadiliko gani yatatokea kwa azma ya Rais Samia kuifumua serikali kama alivyoomba. Azma hiyo haijabainisha ni eneo gani ambalo anakusudia kufumua, hivyo kuwafanya wateule wake kuwa katika hali ya wasiwasi.

Iwapo atadhamiria kweli kufanya mabadiliko makubwa kwa kile alichosema ni kuifumua serikali, maana yake ni kwamba mawaziri na naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri wako katika hofu kubwa ya kukumbwa na fumuafumua hiyo.

Mbali na wateule hao kuwa katika hali ya hofu, wananchi nao wako katika taharuki ya kutaka kujua ni mkeka gani wa wateule utaanza kutolewa na upi utafuata. Pia wananchi hao na hata wateule wanajiuliza swali ambalo halina majibu ya moja kwa moja kwamba je, itafika Krismasi na Mwaka Mpya bila kuwapo mabadiliko?

Aidha, kutokana na taarifa hiyo ya kufumuliwa kwa serikali, baadhi ya wateule kwa maana ya mawaziri na manaibu wao, makatibu wakuu na manaibu wao, wakuu wa mikoa na wilaya, na wakurugenzi wa halmashauri, wameingiwa na hofu huku miongoni mwao wakisherehekea sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka kwa hofu kama wataendelea kuwapo katika timu ya Samia au watatupwa nje.

MBIO URAIS 2025

Kwa muda mrefu tangu Rais Samia aingie madarakani na baadaye kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa, kumekuwa na maneno na minong’ono kuwa kuna kundi ambalo linajiandaa kumpinga katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya chama hicho mwaka 2025.

Licha ya minong’ono hiyo na taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Rais Samia mwenyewe aliwahi kusema kuna watu ndani ya serikali yake wana mipango ya kuwania urais, hivyo akasema ni vyema awaondoe katika safu yake ya uongozi ili wakajiandae vizuri badala ya kuwa nao na matokeo yake wakamhujumu katika jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo.

Jambo hilo alilitimiza mapema mwaka huu alipofanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri  kwa kuwaacha baadhi ya wakongwe waliokuwamo katika awamu zilizopita na ambao walikuwa katika nafasi nyeti.

Mbali na kutekeleza hilo, wakati wa mkutano mkuu uliomalizika majuzi,  Rais mstaafu na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete, Dk. Ali Mohamed Shein, na katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Mzee  Yussuf Makamba, walitoa kauli ambazo zilionyesha kwamba ndani ya chama mambo si shwari hususan mbio kuelekea mwaka 2025.

Viongozi hao bila kuuma maneno, walikemea vikali juu ya watu wanaomendea urais mwaka 2025 na kusisitiza kuwa kama kuna mtu au kikundi cha watu ndani ya CCM waachane na mpango huo. Zaidi  ya hapo, walisema wazi kuwa hakuna mtu ndani ya CCM wa kumpinga Rais Samia utakapofika wakati huo.

KAULI ZA WAZEE

Mbali na mbio za urais ndani ya CCM mwaka 2025, kumekuwa na baadhi ya watu ndani ya chama hicho wanaopinga jitihada za Rais Samia ikiwamo kumkosoa kupitia mitandao ya kijamii na kuleta maneno ya uchochezi.

Hali hiyo iliwaibua wazee, Kikwete, Mzee Makamba na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ambao walitoa kauli nzito dhidi ya watu hao ambao walielezwa kuwa ni watovu wa maadili, hivyo wanapaswa kushughulikiwa na ikiwezekana wachukuliwe hatua kali ikiwamo kufukuzwa uanachama.

Kauli hizo za wazee zimeibua maswali ikiwamo, je wanaodaiwa kumpinga Rais Samia ikiwamo katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2025 wataitwa na kamati ya maadili ya chama na kuchukuliwa hatua?

ANGUKO LA VIGOGO

Uchaguzi wa wajumbe wa NEC kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, umewaacha baadhi ya wadau wa siasa na maswali yasiyo na majibu. Hiyo ni kutokana na baadhi ya vigogo na wakongwe ndani ya chama na serikali kuangukia pua.

Miongoni mwa walioanguka ni mawaziri na naibu mawaziri walioko ndani ya serikali, mawaziri wa zamani na wakuu wa idara za sekretarieti ya CCM. Anguko hilo linaibua swali, je,  mwisho wao wa kisiasa umekaribia?

Habari Kubwa