Mkuu wa JKT ahimiza kuendeleza miradi

30Nov 2020
Hellen Mwango
Morogoro
Nipashe
Mkuu wa JKT ahimiza kuendeleza miradi

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Charles Mbuge, amewaasa maofisa na askari wa Kamandi ya Jeshi la Anga Ngerengere kuondoa ubinafsi na kushirikiana katika kulinda na kuendeleza biashara  ikiwamo miradi ya kukuza uchumi, ili kuchangia pato la taifa kupitia ulipaji kodi.

Alitoa maelekezo hayo mwishoni mwa wiki katika ziara yake ya kikazi katika Kamandi ya Ngerengere ikiwamo kutembelea uwanja wa ndege pamoja na kufungua mradi wa bwalo la Ubena Resort unaotoa huduma kwa maofisa, askari pamoja na wananchi wanaozunguka eneo hilo.

"Sisi kama maofisa wakuu na wadogo pamoja na askari tuondoe ubinafsi, tushirikiane katika kuendesha huu mradi unaotuunganisha na wananchi wanaozunguka itaongeza ukaribu kwa wananchi na jeshi lao la ulinzi," alisema na kuongeza:

"Ninaamini tutachangia uchumi wa nchi kwa kulipa kodi kupitia mradi huu, Suma JKT inachangia Sh. milioni 10 taslimu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba ya kulala wageni ndani ya eneo la bwalo hili, pia nimeagiza Suma kununua mashine ya kufyeka nyasi katika uwanja wa ndege yenye thamani ya Sh. milioni nane badala ya kufyeka kwa mikono.”

Akisisitiza kuhusu nidhamu kwa wanajeshi, alisema serikali ilitoa agizo kwa vikosi vyote kuwa na miradi mbalimbali kwa ajili ya kujiongezea kipato na kupata fedha za kujikimu kwa hiyo badala ya kwenda kupata huduma uraiani wapende vya kwao.

Alisema mbali na fedha za kuanza ujenzi wa nyumba ya kulala wageni, pia ameagiza Suma JKT kuwasilisha kreti 100 za bia na yeye atachangia 50 za soda katika kuinua mtaji wa bwalo hilo.

Alisema Suma JKT iko kwa ajili ya Jeshi na kwamba Sh. milioni 10 alizokabidhi zianze ujenzi mara moja wa nyumba ya kulala wageni waweze kuongeza kipato cha kujikimu.

Meja Jenerali Mbuge alikubali kuwa mshauri na mlezi katika mradi huo kwa kamandi hiyo, pia aliagiza mtaalamu kutoka Suma JKT kwenda kuzungukia eneo hilo mara moja ili waanze ujenzi.

Awali, Mkuu wa Kikosi cha 601, Kanali Zeno Sikukuu, alisema lengo kubwa ni kuboresha huduma za jamii katika eneo linalozunguka bwalo hilo, ikiwamo kuwa na nyumba ya kulala wageni ya kisasa, huduma za kijamii, mashine za kutoa fedha (ATM), maduka ya dawa na mahitaji yote ya kijamii.

Pia alisema wana lengo la kutengeneza maegesho ya magari ya kisasa.

"Afande Mkuu wa JKT, tunaomba ukubali kuwa mshauri wetu wa karibu na  kuwa mlezi wetu katika mradi huu," alisema Kanali Sikukuu.

Naye Mkuu wa Shule ya Anga (SAK), Brigedia Jenerali, Wema Senzia, alisema wana matumaini makubwa ya kufanikisha mradi huo kwa kuzingatia ushauri na kuzingatia maagizo ya mkuu wao.

Mwasisi wa pili wa bwalo hilo, Mwambata wa Kijeshi nchini Ethiopia, Brigedia Mohamed Mohamed, alisema alipohamishiwa kikazi mapema mwaka huu aliona fursa ya kulifufua bwalo hilo, ili kutoa huduma kwa maofisa na askari wanapohitaji kujadili mambo mbalimbali ya kikazi na kijamii.

Kamandi ya Ngerengere inajumuisha vikosi viwili vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha 601 na SAK.

Habari Kubwa