Mkwe wa Mwinyi ataka Ubunge Fuoni

10Dec 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe
Mkwe wa Mwinyi ataka Ubunge Fuoni

MKE wa Mbunge wa Jimbo la Fuoni (CCM) Zubeda Khamis Shaib, amejitokeza kugombea ubunge jimbo la Dimani.

MKE wa Mbunge wa Jimbo la Fuoni (CCM) Zubeda Khamis Shaib.

Uchaguzi mdogo unafanyika kufuatia kifo cha mbunge Hafidh Ali Tahir. Zubeda ni mke wa Abassi Mwinyi, mtoto wa Rais mstaafu, Ally Hassan Mwinyi. Anafanya idadi ya wagombea kufikia 19.

Iwapo Zubeda atashinda katika kura za maoni familia ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi itakuwa na wabunge wanne, watatu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na mmoja Bunge la Afrika Mashariki.

Wabunge hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa jimbo la Kwahani, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Abassi Mwinyi –Fuoni na Abdallah Mwinyi Bunge la Afrika Mashariki.

“Nimechukua fomu ya kugombea ubunge naamini nina uwezo wa kuwatumikia wananchi wa Dimani lengo langu kuondoa changamoto katika sekta ya maji, tiba na miundombinu kwa kushirikiana na serikali iwapo nitachaguliwa.”

Katibu wa Siasa, Uchumi na Fedha wa Wilaya ya Dimani, Juma Nassib Juma, alisema wagombea 19 wamechukua fomu kuwania nafasi hiyo, lakini mpaka jana sita walikuwa wamerejesha akiwemo Mohamed Yusuf Nuh ambaye ni mtaalamu wa masula ya fedha katika Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).

Wabunge wa zamani waliodondoka kwa nyakati tofauti akiwemo Abdallah Sheria(Dimani) Mohamed Rajabu Soud(Jang’ombe) Ameir Ali Ameir (Fuoni) wamechukua fomu za kuwania nafasi hiyo.

Alisema leo Desemba 10 ndiyo mwisho wa kuchukua fomu kwa wagombea kabla ya vikao vya kujadili na kura ya maoni kufanyika kuanzia Desemba 11 kabla ya Kamati Kuu kuteua jina la mgombea mmoja kati ya wagombea watakaopendekezwa na vikao vya CCM Zanzibar.

Aliwataja wagombea wengine waliochukua fomu kuwa ni Juma Ali Juma, Waheed Mohamed Sanya, Jape Ussi Khamis, Aisha Abdalshakur Haji, Mohamed Yusuf Nuh, Naima Ramadhani Pandu, Husseni Ali Najema, Hussen Mgoda, Khatib Abdallah, kuatid Chum Haji, Pandu Juma Mwadini, Asha Suleiman Shaibu, Ibrahim Mbaraka Ramadhan, Silima Khamis Kheir na Mohamed Muhsin Simba.

Uchaguzi mdogo umekuja kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa mbunge wa Dimani Tahr aliyefariki Novemba mwaka huu, akihudhuria vikao vya Bunge Dodoma, lakini mjadala mkubwa umeibuka juu ya CUF na hatima ya kusimamisha mgombea baada ya chama hicho kukumbwa na mgogoro wa uongozi mwaka huu.

Habari Kubwa