Mmiliki kampuni mikopo umiza aingia matatani

17Jan 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Mmiliki kampuni mikopo umiza aingia matatani

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma inamtafuta mmiliki wa kampuni ya ukopeshaji fedha ya mjini Kondoa, Abubakary Kinyuma, baada ya kubainika kushikilia kadi za benki zaidi ya 400 za watumishi mbalimbali, wakiwamo wanaokaribia kustaafu.

Akizungumza jana na waandishi wa habari Jijini hapa, Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Sosthenes Kibwengo, alisema Taasisi hiyo pia inaichunguza kampuni ya mmiliki huyo, ‘Geneva Credit Shop’ baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi 30, wanaodaiwa kupatiwa mikopo umiza na kampuni hiyo.

“Uchunguzi wetu wa awali umeonyesha kwamba pamoja na kampuni hiyo kufanya biashara kwa zaidi ya miaka 25, lakini ilisajiliwa rasmi Oktoba 2016 na hivyo haikuwa inalipa kodi, tumebaini kwamba wengi wakopeshwaji ni watumishi wanaokaribia kustaafu na wamekuwa wakilipishwa riba kubwa kinyume na taratibu za nchi,” alisema Kibwengo.

Alisema Kamati ya Usalama wa Wilaya ya Kondoa, ilifuatilia suala hilo na kufanikiwa kukamata kadi hizo zaidi ya 400 zikiwa zimeshikiliwa na mmiliki huyo ambaye wanamtafuta.

“Mfano mmoja wa waliolalamika kwetu alikopeshwa Sh. 350,000, lakini pamoja na kurejesha Sh. milioni 4.6 alipostaafu mwaka 2018, alikamatwa na mmiliki huyo na kutakiwa kurejesha zaidi ya Sh. milioni 35,” alisema Kibwengo.

Alisema imebainika mmiliki huyo amekuwa na tabia ya kuwaandikisha wadeni wake mikataba kwa nguvu na baadaye kuipeleka mahakamani ili kuhalalisha madai yake.

Wakati huo huo, Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, inatarajia kumfikisha mahakamani, Mhasibu Msaidizi wa Mapato wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Severo Mutegeki (42), kwa tuhuma za kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh. milioni 428....soma zaidi https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa