Mmiliki wa mabasi ya Fikosh atafutwa kulipa gharama za majeruhi

14Sep 2021
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe
Mmiliki wa mabasi ya Fikosh atafutwa kulipa gharama za majeruhi

​​​​​​​NAIBU waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Mwanaidi Khamis, amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanamtafuta na kumpata mmiliki wa kampuni ya Fikosh ambayo inamiliki basi lililopata ajali na kusababisha-

-vifo vya watu watano na majeruhi zaidi ya 30, ili alipe gharama za matibabu za majeruhi wa ajali hiyo.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri huyo baada ya kutembelea majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera na kuelezwa kuwa tangu ajali imetokea mmiliki wa kampuni ya basi lililosababisha ajali, hajawaji kufika hospitalini hapo kuwajulia hali majeruhi hao, ambao baadhi yao wamekatwa mikono.

"Inasikitisha, nasikia mhusika hata kufika kuwajulia hali wagonjwa ameshindwa, naagiza afuatiliwe kwa haraka na aweze kuwahudumiwa waliopata majeraha na wahudumiwe kikamilifu, na pia naagiza tena Hospitali endeleeni kuwapatia huduma majeruhi hawa, ili wapone vizuri maana majengo haya yapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi" amesema Naibu Waziri huyo.

Kaimu RMO Dk. Msereta Nyakiroto (kulia) akitoa maelezo kwa Naibu WAziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwanaidi Khamis (kushoto).

Mmoja wa majeruhi wanaondelea na matibabu katika Hospitali hiyo Nobert Philbert, ambaye amekatwa mkono wa kushoto, amesema kuwa tangu ajali hiyo imetokea ni takriban siku tisa sasa, na kwamba wamekuwa wakijigharamia wenyewe matibabu lakini wameishiwa fedha na kuomba serikali kuwasaidia.

"Mimi na familia yangu tumekuwa tukitafuta gharama za matibabu wenyewe, wakati mwingine tunaomba misaada kwa watu lakini tunakoelekea hatutaweza kuendelea kupata fedha, na mimi kama mnavyoona nimekatwa mkono hata nikikopa sina tena uwezo wa kufanya kazi na kuingiza kipato, ili nilipe madeni baada ya kuruhusiwa" amesema Nobert.

Kaimu Mganga Mkuu mkoani humo Dk. Msereta Nyakiroto ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri, na kuahidi kulifanyia kazi haraka agizo walilopewa.

Basi la kampuni ya Fikosh lenye namba za usajili T710 BXB ambalo hufanya safari zake kutoka mkoani Kagera kwenda mkoani Mwanza, lilipata ajali Septemba 05 mwaka huu wakati likitoka mkoani Mwanza na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi zaidi ya 30 .