Mnunuzi Lugumi alivyoweka historia

14Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mnunuzi Lugumi alivyoweka historia

‘MNUNUZI’ wa nyumba za kifahari za kampuni ya Lugumi Enterprises, Dk. Louis Shika, ameweka rekodi ya aina yake baada ya kuingia kwenye orodha adimu ya watu waliojadiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii mpaka sasa mwaka huu, kutokana na matukio mbalimbali.

Dk. Louis Shika akipongezwa na mkurugenzi wa Yono Christina Kevela kwa kununua nyumba za lugumi.

Leo ni siku ya tano tangu Dk. Louis aibue kioja cha kutaka kununua nyumba tatu za Lugumi kwa jumla ya Sh. bilioni 3.3 huku akishindwa kutoa asilimia 25 ya kiasi hicho kama kanuni za mnada zinavyotaka.

Anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, na hilo limefanya awe gumzo zaidi kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na habari zake pia kuandikwa magazetini.

Dk. Shika anakuwa mtu wa tatu kujadiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii, baada ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu na Mbunge wa Shingida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Mjadala kuhusu Lissu ulishika kasi kwenye mitandao ya kijamii kwa siku kadhaa baada ya kupigwa risasi 32 na watu wasiojulikana Septemba 7 akiwa nje ya nyumbani yake mjini Dodoma na baadaye kulazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Aidha, Oktoba 30 Nyalandu alitangaza kuihama CCM na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo, hatua ambayo iliibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii hadi kufikia watu kutumiana ujumbe mbalimbali wa kejeli.

VIJIWE VYA KAHAWA
Tangu ashinde kwenye mnada wa kununua nyumba hizo za kifahari kwa thamani ya jumla ya Sh. bilioni 3.3 Alhamisi iliyopita, Dk. Shika amekuwa hakauki kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, WhatsApp na Instagram.

Mjadala huo unafuatia nia yake ya kutaka kununua nyumba hizo za kifahari zilizoko Mtaa wa Mazengo Upanga, na mbili zilizoko Mbweni JKT, jijini Dar es Salaam.

Dk. Shika amekuwa mjadala si tu kwenye mitandao ya kijamii bali hata kwenye mikusanyiko kama vijiwe vya kahawa na kwenye ofisi mbalimbali watu wakijadili ilikuwaje atamani kununua nyumba za kifahari wakati akijua hana fedha.

Tukio hilo la Dk. Shika lilianza kuwa maarufu mitandaoni mchana wa siku hiyo ya mnada, Novemba 9, hivyo kufunika mjadala uliokuwa umebamba wakati huo wa Nyalandu, aliyekihama Chama Cha Mpinduzi.

Kauli ya Dk. Shika kwamba "900 itapendeza zaidi" akimaanisha anaahidi kununua nyumba kwa Sh. milioni 900 aliyoitoa siku ya mnada huo, ndiyo inaendelea kubamba kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakituma picha mbalimbali zilizoandikwa '900 itapendeza zaidi'.

Kadhalika, picha tofauti tofauti za kutengenezwa zimekuwa zikitumwa kwenye mitandao hiyo zikimuonyesha Dk. Shika akiwa na watu mashuhuri na wafanyabiashara wakubwa duniani kama Bill Gates na wengine.

Nipashe ilipotembelea makazi yake Tabata Mawenzi, ilibaini kuwa Dk. Shika anaishi kwenye chumba kimoja ambacho anakilipia Sh. 50,000 kwa mwezi.

Mmoja wa wapangaji wenzake ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema Dk. Shika anaishi maisha magumu na kuna wakati wapangaji wake wanamsaidia chakula.

WAFUASI WA CCM
Mjadala kuhusu hatua ya Nyalandu kukihama chama chake na kwenda Chadema, ulitawala kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha mnyukano kupitia jumbe mbalimbali zilizokuwa zinatumwa.

Waliokuwa wanapambana kwenye mitandao hiyo ni wale wanaoonekana kuwa makada na wafuasi wa CCM, wafuasi wa Chadema na wengine wenye mwelekeo wa uanaharakati ambao walionekana kuunga mkono uamuzi huo.

Baadhi ya walioonekana kuiunga mkono CCM walikuwa wakirusha maneno ya kumdhihaki Nyalandu na kumwonyesha kama mtu ambaye alikuwa amechokwa ndani ya chama hicho hivyo kuondoka kwake hakutaathiri chama kwani walishapanga kumtimua.

Waliokuwa wanamuunga mkono Nyalandu walikuwa wakiwajibu wenzao kuwa kama alikuwa fisadi ilikuwaje akadumu kwenye chama hicho hadi pale alipoamua mwenyewe kukihama chama hicho na kupita kwenye mchujo wa kura za maoni kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.