Mnyika ataka mabadiliko ya Katiba mkutano ujao Bunge

13Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mnyika ataka mabadiliko ya Katiba mkutano ujao Bunge

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, ametaja maeneo manne ya kwenye Katiba yanayohitaji marekebisho.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, picha mtandao

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema ipo haja kwa Rais John Magufuli kupeleka marekebisho ya katiba kwenye kikao cha bunge kinachotarajiwa kuanza Januari 28, mwaka huu.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, matokeo ya uchaguzi wa Rais kupingwa mahakamani, mgombea urais kupata zaidi ya asilimia 50 (50%+1) na wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kupigiwa kura ya ndiyo au hapana inapotokea kuna mgombea mmoja, badala ya sasa ambapo hupita bila kupingwa.

Kwa mujibu wa Mnyika, marekebisho hayo yatakuwa mwarobaini wa kuepusha uhasama, vurugu na mtanziko wa kisiasa unaotokana na kuvurugwa kwa uchaguzi nchini, kama ilivyotokea Zanzibar mwaka 2015.

Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, alisema maeneo muhimu yanayohusu uchaguzi ili wapigakura, wapate fursa ya kuchagua viongozi bora kupitia sanduku la kura kwa ajili ya maendeleo ya wote.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alitoa maagizo kwa wabunge wa Chadema kwa kushirikiana na wabunge wengine wa upinzani bungeni kuhakikisha kuwa agenda ya marekebisho ya uchaguzi inapewa uzito na kipaumbele kwenye mkutano wa 18.

Alisema mchakato huo uanzie kwenye vikao vya Kamati za Bunge ambavyo vimepangwa kuanza vikao vyake Januari 13, mwaka huu, huku vikao vya Bunge zima vikipangwa kuanza Januari 28, mwaka huu.

Katibu Mkuu Mnyika alisema maeneo ambayo Katiba inapaswa kufanyiwa marekebisho ya haraka kukidhi matakwa na maslahi ya Watanzania wakati taifa linaelekea kufanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ili kuhakikisha kuwa haki ya wapigakura kuchagua viongozi bora wanaowataka haipokwi wala kuchezewa.

“Mswada huo wa marekebisho ya Katiba ulenge kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, uchaguzi wa urais kupingwa mahakamani, mgombea urais kushinda kwa kupata kura zaidi ya asilimia 50 na wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kupigiwa kura za ndiyo au hapana kama ilivyo kwa mgombea wa urais,” alisema na kuongeza:

“Inapotokea kuwa mgombea wa ubunge au udiwani yuko peke yake. Tusiruhusu masuala ya watu kupita bila kupingwa ambayo ndiyo yanawasaidia wakurugenzi na wasimamizi wa uchaguzi kukimbia ofisi kukwepa kuteua wagombea wa upinzani.”

Aidha, alisisitiza kuhusu tume huru ya uchaguzi nchini, amesema kuwa umuhimu wa suala hilo si kwa ajili ya vyama vya siasa pekee, hivyo ametoa wito kwa wadau wengine, asasi za kiraia nchini, madhehebu na viongozi wa dini nchini na makundi mengine mbalimbali nchini kuungana katika jambo.

Habari Kubwa