Mnyukano kisheria kesi Bilionea Msuya

14Nov 2017
Godfrey Mushi
Nipashe
Mnyukano kisheria kesi Bilionea Msuya

MNYUKANO wa kisheria umeibuka katika Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi kuhusu nani kati ya upande wa utetezi na upande wa mashtaka mwenye uwezo wa kutoa nyaraka yenye malezo ya shahidi mahakamani katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara tajiri wa madini ya tanzanite, Erasto Msuya (43).

Mabishano hayo yaliibuka jana, baada ya shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka, Elirehema Msuya maarufu Kakaa ambaye ni dereva wa Hoteli ya SG Resort iliyopo Sakina mjini Arusha, kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza shauri hilo, namba 12 la mwaka 2014.

Shahidi huyo, wakati anahojiwa na upande wa utetezi aliulizwa swali na wakili Majura Magafu anayemtetea mshtakiwa wa pili na wa tano, kama anataka maelezo yake yatolewe mahakamani kama kielelezo na hapo ndipo upande wa mashtaka ulipopinga kutolewa kielelezo hicho, ukidai Magafu hana uwezo wa kutoa nyaraka hiyo mahakamani isipokuwa shahidi.

Akitetea hoja yake ya kutaka mahakama ipokee kielelezo hicho, Magafu alidai kuwa kifungu cha 154 na kifungu cha 164 cha Sheria ya Ushahidi, vimewekwa makusudi kwa ajili ya pindi mkanganyiko unapojitokeza na kwamba pingamizi la upande wa mashtaka halina miguu ya kusimamia.

Akiijenga hoja yake, wakili Magafu alidai kwamba, kwa mujibu wa matakwa ya kifungu cha 154 na kifungu cha 164 vya Sheria ya Ushahidi, maelezo ya shahidi yanaweza kutolewa na upande mwingine ili kuonyesha kutoendana na maelezo ya awali yaliyoandikwa polisi.

“Shahidi mwenyewe aliyepo kizimbani kakubali statement (maelezo) ni ya kwake, pingamizi linalotolewa na Prosecution (upande wa mashtaka) halina mantiki na linapingana na kifungu cha 154 na 164 of Evidence Act (Sheria ya Ushahidi), hivyo tunaomba statement hii ipokee kama kielelezo,”alidai Magafu.

Baada ya ombi hilo la Majura, Wakili wa Serikali, Kassim Nassir alisimama na kuieleza mahakama hiyo kwamba upande wa mashtaka unapinga kupokelewa kwa maelezo ya shahidi wao kwa sababu shahidi hajaiomba mahakama hiyo maelezo yake yatolewe kama kielelezo, isipokuwa aliyeomba maelezo yapokelewe ni wakili Magafu.

Hoja hiyo ikamwinua Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdala Chavula na kuieleza mahakama hiyo ni msimamo wa sheria kwamba anayetakiwa kuingiza nyaraka mahakamani ni lazima awe halali, kwa kuwa Magafu siyo shahidi na hajaapishwa kama shahidi.

Chavula alidai: “Tunaambiwa utaratibu ni exptional to the general rule (kuna mazingira yanaweza kutumika ukiachia kanuni zinazoongoza upokelewaji wa maelezo), lakini mahakama hii haijaelekezwa ni sheria gani inayotoa hiyo exptional (mazingira tofauti). Kifungu cha 154 kikisomwa na kifungu cha 164 (1), vinatoa nafasi ya wakili ambae si sehemu ya ushahidi kutoa document.

"Kifungu cha 154 ukianzia nacho chenyewe, hakitoi nafasi hiyo, badala yake kinatoa haki ya kum-contradict (kumpinga) shahidi na maelezo yake aliyoyatoa kulingana na alichokizungumza awali. Kifungu cha 164 (1) nacho vile vile hakitoi hayo ambayo wakili Magafu anataka mahakama iamini kwamba yapo.”

Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, mwaka 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kandokando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, 'Mredii' (38), mkazi wa Songambele wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai Kwa Mrefu.

Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Jabir a.k.a Msudani (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, wilaya ya Hai, Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu Majeshi, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.

Baada ya malumbano hayo ya kisheria, Jaji Salma aliahirisha shauri hilo kwa ajili ya kutoa uamuzi mdogo kuhusu pingamizi la upande wa mashtaka kutaka kielelezo hicho kisipokelewe.

Awali, kabla ya kuibuka malumbano hayo, Wakili wa Serikali, Kassim Nassir alimuongoza shahidi huyo wa 13 kutoa ushahidi wake kizimbani na mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Nassir: Unafanya shughuli gani?
Shahidi: Mimi ni dereva.

Wakili Nassir: Hiyo shughuli yako ya udereva unaifanyia wapi?
Shahidi: SG Resort (hoteli).

Wakili Nassir: Hiyo SG Resort iko wapi?
Shahidi: Iko Sakina, Arusha.

Wakili Nassir: Shahidi hebu tueleze tarehe 6/8/2013 siku hiyo ulikuwa wapi?
Shahidi: Nikuwa Hotelini SG Resort.

Wakili Nassir: Sasa hebu ieleze mahakama hii siku hiyo ulifanya nini?
Shahidi: Niliendesha gari kutoka SG Resort kwenda mjini (Arusha) kufanya purchasing (manunuzi) na niliporudi nilimwona marehemu akiongea na mtu.

Wakili Nassir: Nini kiliendelea baada ya wewe kupaki gari?
Shahidi: Nilimwona marehemu Erasto Elisaria Msuya akiendelea kuongea na huyo mtu.

Wakili Nassir: Huyo Erasto ni nani katika hiyo hoteli?
Shahidi: Ni mmiliki.

Wakili Nassir: Wakati unamuona marehemu anaongea hapo kwenye swimming pool, wewe ulikuwa unafanya nini?
Shahidi: Nilikuwa nimepaki gari na niko hapo.

Wakili Nassir: Walikaa hapo kwa muda gani?
Shahidi: Kama dakika 20 hivi.

Wakili Nassir: Baada ya hapo walifanya nini?
Shahidi: Waliamka na kuingia ndani hotelini, lakini sikujua walikwenda kukaa upande gani.

Wakili Nassir: Walipotoka nini kiliendelea?
Shahidi: Marehemu Erasto aliniita Kakaa uko wapi... Nilimjibu niko huku parking (kwenye maegesho), akaniambia washa gari, nikamuuliza la kwangu au la kwako akanijibu la kwako, basi mimi nikawasha gari nikawasogelea mpaka walipokuwa wamesimama marehemu na huyo.

Wakili Nassir: Halafu ikawaje baada ya kuwasogelea?
Shahidi: Marehemu aliniambia mgeni wangu huyu, mpeleke stendi ya mabasi ya Arusha/Moshi na hakikisha unampandisha kwenye Costa na usimteremshe njiani, nikamwambia sawa.

Wakili Nassir: Kitu gani kingine alimwambia huyo mtu?
Shahidi: Marehemu alimwambia huyo mtu kwamba hakikisha unamhimiza huyo ndugu yako tumalize hiyo biashara kesho asubuhi Bomang’ombe.

Wakili Nassir: Huyo mtu akajibuje?
Shahidi: Akasema sawa brother (kaka).

Wakili Nassir: Sasa baada ya kufika stendi ilikuwaje wewe na huyo mtu?
Shahidi: Tulivyofika hakutaka nimtafutie Costa, alisema yeye anapajua vizuri hapo na akaniambia nimshushe na baada ya kushuka aligeuka nyuma na kuniaga akiniambia tutaonana kesho.

Wakili Nassir: Huyo mtu aliyekuwa na marehemu, leo unaweza kumkumbuka hapa mahakamani?
Shahidi: Ndio.

Wakili Nassir: Kabla ya tarehe 6/8/2013 ulishawahi kumuona?
Shahidi: Hapana, sikuwahi.

Wakili Nassir: Ulishawahi kuwa na ugomvi nae siku za nyuma?
Shahidi: Hapana.

Wakili Nassir: Baada ya kurudi hotelini nini kiliendelea?
Shahidi: Nilimkuta marehemu Erasto ameshaondoka.

Wakili Nassir: Nini kilitokea tarehe 7/8/2013?

Shahidi: Siku hiyo kwenye majira ya saa nne asubuhi marehemu alinipigia simu na kuniambia Kakaa uko wapi, nikamjibu niko hapa hotelini, akaniambia nenda kwa Meneja mwambie akupe Sh. milioni moja, halafu nimemwagiza mtoto gari aniletee, njoo nalo hadi hapa Philips.

Wakili Nassir: Alikwambia amemwagiza mtoto gani hilo gari?
Shahidi: Ni mtoto wake anaitwa Glory.

Wakili Nassir: Ni gari gani hilo aliloagiza aletewe?
Shahidi: Range Rover.

Wakili Nassir: Alipokuja huyo mtoto ulifanya nini?
Shahidi: Nilichukua ile Sh. milioni moja na gari nikamfuata marehemu Philips.

Wakili Nassir: Ulipofika na kumpa hela na hilo gari nini kiliendelea?
Shahidi: Aliniambia naenda KIA kufanya biashara narudi sasa hivi.

Wakili Nassir: Nini kilitokea ukiwa mjini?
Shahidi: Yule mwenzangu anaitwa Rama alipigiwa akanambia umesikia Erasto amepigwa risasi huko maeneo ya Mijohoroni, KIA?

Baada ya Wakili Nassir kumaliza kumuongoza, wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo alianza kumfanyia mahojiano shahidi huyo na mambo yakilikuwa hivi:

Wakili Ndusyepo: Shahidi una elimu gani katika madarasa?
Shahidi: Kidato cha nne.

Wakili Ndusyepo: Umesoma shule gani?
Shahidi: Makumira Sekondari.

Wakili Ndusyepo: Kabla ya kazi ya udereva ulikuwa unajishughulisha na nini?
Shahidi: Uchimbaji wa madini Mererani.

Wakili Ndusyepo: Unaweza kukumbuka huyo mgeni wa marehemu Erasto alivaaje siku hiyo?
Shahidi: Huyo mgeni wa marehemu alikuwa amevaa kofia ya kapelo.

Wakili Ndusyepo: Alikuwa amevaa mavazi gani mengine?
Shahidi: Sikumbuki.

Wakili Ndusyepo: Watu ulioitwa kuwatambua siku ile ya gwaride walikuwa wangapi?
Shahidi: Idadi yao sikumbuki.

Wakili Ndusyepo: Unakumbuka namba za usajili za ile Range Rover?

Shahidi: Ni T800 CKF.

Wakili Ndusyepo: Hivi marehemu alikuwa na tabia ya kutembea na silaha?
Shahidi: Najua alikuwa na bastola.

Wakili Ndusyepo: Siku uliyoenda kwenye gwaride Polisi walikuambia huyo mtu unayekwenda kumtambua amepangwa mtu wa ngapi?
Shahidi: Sikuambiwa.

Dakika chache baadaye wakili Magafu alipokea kijiti hicho na kuanza kumhoji shahidi huyo na mahojiano hayo yalikuwa hivi:

Wakili Magafu: Hebu tusaidie ni nani aliyekwambia unatakiwa kwenda kwenye gwaride la utambulisho wa mtu aliyemuua marehemu?
Shahidi: Waliniambia nikamtambue mtu niliyempeleka stendi.

Wakili Magafu: Utakubaliana na mimi kwamba wewe hujui kutambulisha rangi ya mtu?
Shahidi: Najua.

Wakili Magafu: Maelezo yako umeandika mara ngapi?
Shahidi: Mara mbili.

Wakili Magafu: Haya maelezo yako uliandika ukiwa sehemu gani?
Shahidi: Central (Kituo Kikuu cha Polisi) Arusha.

Wakili Magafu: Gwaride la utambulisho lilifanyika saa ngapi?
Shahidi: Ilikuwa jioni.

Wakili Magafu: Hilo gwaride la utambulisho lilichukua takribani dakika ngapi?
Shahidi: Lilichukua kama dakika tatu hivi.

Wakili Magafu: Hilo gwaride lilifanyikia sehemu gani?

Shahidi: Kwa RCO (Mkuu wa Upelelezi Mkoa), kwenye uwanja wa wazi.

Jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo linaongozwa na wakili Ndusyepo anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Magafu anayemtetea mshtakiwa wa pili na wa tano, Emmanuel Safari anayemtetea mshtakiwa wa tatu na John Lundu anayemtetea mshtakiwa wanne, sita na saba.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Chavula.

Hadi sasa jumla ya mashahidi 12 wa upande wa mashtaka, wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo.

Habari Kubwa