MO afunguka kutekwa kwake

01Jun 2019
Romana Mallya
DAR
Nipashe
MO afunguka kutekwa kwake

MFANYABIASHARA maarufu nchini Mohamed Dewji (44), maarufu kama MO, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu kutekwa kwake mwishoni mwa mwaka jana.

Mohamed Dewji.

MO ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kundi la Kampuni za MeTL (MeTL Group) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, amesema ana deni kwa taifa na Watanzania kwa ujumla kwa kwa kuwa walionyesha kuguswa na tukio hilo.

Aliyasema hayo juzi usiku jijini Dar es Salaam wakati wa tuzo alizoandaa kwa ajili ya Klabu ya Simba ziitwazo ‘MoAward2019’ zilizotolewa kwa wachezaji wa klabu hiyo ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tuzo hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza kwenye sherehe hizo, MO alisema ndani ya msimu huo uliomalizika wa Ligi Kuu Tanzania Bara, alipata msukosuko wa kutekwa lakini alisalimika kwa kudra za Mwenyezi Mungu na kupitia maombi ya Watanzania.

MO alitekwa Oktoba 11, mwaka jana na watu wasiojulikana wakati akienda kufanya mazoezi ya viungo katika hoteli ya Colleseum iliyoko Oysterbay, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Alitekwa muda mfupi baaada ya kushuka kwenye gari lake lililosajiliwa kwa jina la MO 1 nje ya hoteli hiyo saa 11:00 alfajiri.

“Ndani ya msimu huu uliomalizika wa Ligi Kuu Tanzania Bara, nilipata msukosuko wa kutekwa lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu na kupitia maombi ya Watanzania niliweza kusalimika na jambo hili. Namshukuru Mungu,” alisema MO na kuongeza:


“Hakika katika jambo hili ndipo nilipofahamu mapenzi ya Watanzania kwangu. Waliniombea bila kujali tofauti za dini na itikadi. Nina deni na nchi yangu, nina deni na Watanzania. Ninasema asanteni sana kwa dua zenu.”

MO ni mfanyabiashara kijana anayeongoza kwa utajiri Afrika, ambaye pia mwaka 2017 jarida maarufu duniani la Forbes lilimtaja kuwa tajiri wa 16 barani Afrika.


Jrida la Forbes liliwahi kukadiria kuwa mfanyabiashara huyo ana utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.5 unaomfanya ashike nafasi ya 1,500 duniani na nafasi ya 31 Afrika kwa mwaka 2015.

Habari Kubwa