Mo Dewji atunukiwa  PhD Marekani 

22May 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Mo Dewji atunukiwa  PhD Marekani 

MFANYABIASHARA Bilionea Mohammed Dewji, maaryfu MO, ametunukiwa udaktari wa falsafa (PhD) na Chuo Kikuu cha Georgetown McDonough School of Business cha Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa leo Maei 22,2022 kwenye tovuti ya chuo hicho kilichoko Washington D.C, Rais wa Chuo Kikuu cha Georgetown, John DeGioia ndiye aliyemtunuku MO Dewji PhD ya heshima Ijumaa iliyopita chuoni huko kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii ya Tanzania.

MO Dewji ambaye mbali na biashara, amewekeza kwenye michezo, ni Mkurugenzi Mtendaji wa MeTL Group na Mwasisi wa Taasisi ya Mo Dewji ambayo inatoa huduma za hisani ikiwamo katika sekta za elimu na afya.

MO Dewji alihitimu katika Chuo Kikuu hicho cha Georgetown McDonough School of Business mnamo mwaka 1998 na aliporejea nchini aliitumia elimu ya biashara aliyoipata huko na kuipa mafanikio makubwa MeTL Group.

 “Tunampongeza na anastahili heshima hii  heshima hii," chuo hicho kilitamka kupitia taarifa hiyo iliyoambatanishwa na picha za MO Dewji akitunukiwa PhD na alipohutubia kwenye mahafali ya chuo hicho Ijumaa iliyopita.

Katika hotuba yake wakati mahafali hayo, MO Dewji aliwataka wahitimu na wanafunzi wanaoendelea na masomo chuoni huko, kuzingatia misingi ya biashara, akisema: "Dunia siyo yako -- lakini siku zote inakuhusu"

 MO Dewji alisisitiza umuhimu wa kutumia watu wanaokuzunguka, kujitolea kwa wengine na kujenga jamii iliyo imara.

Aliwataka wanafunzi 776 wanaoendelea na masomo na wahitimu 330 katika Shule ya Biashara ya McDonough ya chuo kikuu hicho kwa kukumbuka umuhimu wa kubadilishana mawazo kwa lengo la kuwajibika kwa jamii ba kumjali kila mtu.

Pia aliwataka wanafunzi kutotoka nje ua misingi muhimu wanapoendelea na masomo yao, pia watakapokuwa wanatekeleza kwa vitendo walichokisomea. 

“Sina shaka na yeyote kati yenu katika kuzingatia misingi hiyo," MO Dewji alisema na kutoa angalizo kwamba: Tambueni hili -- kadri unavyofanikiwa, ndipo inapokuwa rahisi zaidi kwako kusahau namna unavyoihitaji jamii yako".

Katika orodha ya mwaka huu ya mabilionea duniani iliyotolewa na jarida maarufu la biashara la Forbes, Mo Dewji ameendelea kung'ara akiwa bilionea namba moja Tanzania na Afrika Mashariki, pia akiingia kwenye orodha ya mabilionea barani Afrika.

Kwa mujibu wa Forbes, Mo Dewji kwa sasa anashika nafasi ya 15 kwenye orodha ya mabilionea barani Afrika akiwa na utajiri unaofilia Dola za Marekani bilioni 1.5.

Habari Kubwa