MO Dewji amwahidi Samia ajira 100,000

25Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
MO Dewji amwahidi Samia ajira 100,000

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mohamed Dewji 'MO Dewji', amebainisha kufurahishwa na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha uwekezaji na biashara nchini.

Katika kuunga mkono jitihada hizo, MO Dewji ameahidi kuwa katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Samia, ataongeza ajira kutoka 31,000 za sasa hadi 100,000.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Kampuni ya Mohamed Enterprisses (MeTL), aliahidi hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaofadhiliwa na Taasisi yake (MO Dewji Foundation).

Alisema Rais Samia amerejesha uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali na wawekezaji, jambo analoamini litasaidia kukua kwa uchumi wa taifa, mtu mmoja mmoja na kuongeza ajira.

“Kuna mwelekeo mzuri chini ya Rais Samia, ninawaomba wafanyabiashara wenzangu tumuunge mkono Rais wetu kwa kuwa anataka tupige hatua na kukuza uchumi," alisema.

MO Dewji alisema Rais Samia anafanya vizuri katika kuwavutia wawekezaji wa nje na kuwalinda, hivyo anaamini baada ya miaka michache uchumi wa Tanzania utaimarika zaidi.

Kuhusu ufadhili wa MO Dewji Foundation kwa wanafunzi hao takriban 100, MO Dewji alisema ulianza mwaka 2015 na kadri siku zinavyokwenda ndivyo anavyoongeza zaidi idadi ya wanufaika, akilenga kuwafikia 10,000 katika miaka mitano ijayo.

Aliwataka wanufaika hao kuendelea kumwombea kwa kuwa anapitia wakati mgumu kwenye maisha yake.

"Mimi ninawaomba mkishafanikiwa mkumbuke kuwasaidia na wengine kwa kuwa mimi sitaki mnirejeshee hata senti moja, lengo langu ni kuhakikisha tunapiga hatua na kuondokana na umaskini," alisema.

Bilionea huyo kijana zaidi Afrika, alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, zaidi ya Sh. bilioni moja zimetumika katika mradi huo wa kuwafadhili wanafunzi vyuoni ili wafikie ndoto zao.

“Uhitaji ni mkubwa lakini tunaangalia zaidi wale wanaotoka katika mazingira magumu bila upendeleo wowote, tunazingatia usawa kijinsia na hata dini," alisema.

Miriam Ibrahim, mmoja wa wanufaika hao, aliishukuru taasisi hiyo kwa kuwasaidia kufikia ndoto zao.

“Tumekuwa tukipata fursa mbalimbali kupitia taasisi hii ikiwamo wengine kupata kazi katika kampuni ya MeTL. Ninatoa wito kwa taasisi zingine kuiga mfano huu," alisifu.

Baraka Edward, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema: “Tukisema tukulipe kwa kile ambacho umekifanya hatuwezi. Hata tukisema tuje kufanya kazi bure katika kampuni yako haiwezi kulipa jinsi ulivyotusaidia. Mungu akubariki sana, Asante MO!"

Katika mkutano wake huo na wanafunzi hao, MO Dewji pia alikumbusha kuhusu tukio la kutekwa kwake lililotokea Oktoba 11, mwaka juzi kwenye Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

"Lazima nimshukuru Mungu, nina deni kubwa na nchi hii. Ninajua mnajua mimi nilitekwa siku tisa, nilikuwa najua nakufa, lakini Watanzania waliniombea na Mungu akawasikia.

"Nina deni kwa Watanzania ndiyo maana sitaacha kujitolea kila nilichonacho kwa ajili yao," MO Dewji alihitimisha.

Habari Kubwa